Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online, Dar
WATOTO wanaoishi na kufanyakazi mitaani waliogeuza kituo cha mabasi yaendayo mikoani Ubungo kama sehemu ya kudumu ya malazi yao, wamesema hawajui hatima yao Stendi hiyo itakapohamishiwa Mbezi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam wiki hii.
Watoto hao wamesema tayari waliishaanza kuona nuru ya kufikia ndoto yao tangu waanze kusaidiwa na asasi ya Railway Children Africa inayotekeleza Mradi wa USAID-Kizazi Kipya kwa kushirikiana na Taasisi ya Baba Watoto.
Wakizungumza na Majira mwishoni mwa wiki kwa nyakati tofauti, watoto hao walimuomba Rais John Magufuli anayetarajia kuzindua stendi kusikia kilio chao kwa kuwatafutia makazi yenye malazi salama, wakati wakiendelea kusaidiwa ili kufikiwa ndoto zao.
Akizungumza kwa sharti la kutotaja jina, mmoja wa watoto hao amesema pamoja na msaada mkubwa wanaoupata, lakini kikwazo kikubwa imekuwa ni sehemu ya kulala.
“Tumeambiwa Stendi ya Mbenzi kutakuwa na ulinzi mkali, hatuwezi kupata malazi pale hii inaweza kutufanywa tushindwe kupata kile ambacho tumeanza kusaidiwa,” amesema matoto kwa niaba ya watoto wenzake.
Amesema Mradi wa USAID- Kizazi Kipya umeweza kufufua ndoto zao, kwani kila siku kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa wanafika Kituo cha Mburahati Baba Watoto, ambapo wanapatiwa huduma muhimu.
Miongoni mwa huduma hizo ni pamoja na kupimwa afya zao, kwa wanapougua wanapelekwa hospitali na kupatiwa matibabu. Huduma nyingine ni chakula, maji ya kuoga, sabuni na wanapelekwa VETA kupata elimu ya ufundi na kwenye gereji za watu binafsi.
Mtoto mwingine (jina tunalo) amesema changamoto kubwa imekuwa ni kutoruhusiwa kulala kwenye Kituo cha Baba Watoto Mburahati, hivyo ikifika saa 9 alasiri kila mmoja anarudi anapoishi na
kufanyakazi mtaani kwa ajili ya kusubiri ratiba ya siku inayofuata.
“Sasa Stendi inahama Ubungo na Mbenzi tunaambiwa kutakuwa na ulinzi, tunamuomba mzazi wetu Rais Magufuli alione hili ili tuwe na sehemu salama ya kulala wakati tunaposaidiwa kufikia ndoto yetu kupitia mradi wa USAID-Kizazi Kipya,” amesema mtoto huyo.
Amesema katika Stendi ya Ubungo kuna kundi kubwa la watoto ambao wanapata msaada mkubwa kutoka Railway Children Africa kwa kushirikiana na Taasisi ya Baba Watoto, lakini ndoto zao zinaweza kurudishwa nyuma kama hawatapata makazi ya salama kwa ajili ya malazi.
Akizungumza na Majira, Afisa Mawasiliano wa Railway Children Africa, Henry Mazunda amekiri watoto hao kukabiliwa na changamoto ya malazi, hali inayowalazimu kutorudi wanapoishi na kufanyakazi mara baada ya ratiba ya kukaa kituoni kumalizika.
Amesema watoto hao wanapokuwa mitaani wanakabilia na changamoto nyingi, ikiwemo ukatili wa aina nyingi na wakati mwingine kujikuta wakikamatwa na Polisi na hata kukaa muda mrefu vituoni bila kupelekwa Mahakamani.
Mazunda amesema taasisi hiyo ina wakili na imekuwa ikishirikiana na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kwa ajili ya kuwapatia msaada wa kisheria.
Amesema wamekuwa wakifanyakazi zao kupitia ngazi tatu. Amesema ngazi ya kwanza ni ya kuwafuata watoto wanaoishi na kufanyakazi mitaani na kuwapatia mahitaji muhimu na ya haraka.
Ametaja mahitaji hayo kuwa ni pamoja na msaada wa kisheria, chakula na kufanya jitihada za kuwaunganisha na familia zao pamoja na kuendelea kuwapatia mahitaji yao muhimu ikiwemo chakula pamoja na mahitaji ya shule.
Ngazi nyingine ni kuelimisha jamii ili iweze kutambua kuwa watoto
wanaoishi na kufanyakazi mitaani wana haki sawa na watoto wengine,
hivyo hawana sababu ya kuwaona kama watu wabaya.
“Watoto hawa wanaondoka nyumbani kwa sababu mbalimbali ikiwemo wazazi kutengana, kukosa mahitaji maalum kwa sababu za umasikini, pamoja na ukatili, kwa hiyo watoto hawa wanahitaji kusaidiwa,”amesema.
Amesema taasisi hiyo inafanyakazi katika mikoa saba nchini na tayari imeishahudumia watoto zaidi ya 10,000.
More Stories
Bodi ya NHIF yatakiwa kutatua changamoto za wanachama wake
Rais Samia, Mwinyi ‘mitano tena’ Nchimbi aula
Dkt.Kikwete:Ushindi wa CCM ni lazima