November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

STAMICO yajinasibu kukusanya bilioni 4.1 kwa mwezi

Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online,Songwe

SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) linalochimba madini ya makaa ya mawe kupitia mlima Kabulo limejinasibu kukusanya kiasi cha bilioni 4.147 kwa mwezi baada ya kufunga mitambo mipya huku wananchi wanaozunguka mgodi huo wakianza kunufaika..

Shirika hilo baada ya kusimama kutoa huduma miaka ya nyuma limeanza tena kufanya kazi ya uzalishaji kwa kufunga mitambo mipya inayorahisisha kuchakata makaa ya mawe.

Baada ya mgodi huo kuanza kuzalisha kwa kasi jitihada mbalimbali za kuuboresha zimeanza na hata viongozi mbalimbali wa kitaifa,kimkoa na kiwilaya wamekuwa wakiutembelea mradi huo na kuona kasi ya uzalishaji.

Ombi kubwa la wadau wa maendeleo ni kuona majengo pia yakiboreshwa kwani yamechakaa licha ya awali majengo hayo yakiwa katika ubora picha zake zilitumika kwenye baadhi ya noti za kitanzania ikiwemo noti ya Tsh,1,000.

Siku za hivi karibuni,Mkuu wa mkoa Songwe Daniel Chongolo alifanya ziara ya kuutembelea mgodi huo akiwa na timu nzima ya usalama ya Mkoa na wakuu wa taasisi ambapo alitoa ushauri kwa Maofisa wa Stamico ili wazalishe kwa tija makaa hayo ya mawe ambayo kwa sasa soko lake ni kubwa ukilinganisha na ilivyokuwa awali.


Sambamba na kutoa ushauri huo Chongolo amewataka viongozi wa mgodi huo kuharakisha ujenzi wa majengo muhimu mgodini hapo ili tija zaidi ya uzalishaji ifanyike na kutaka mgodi huo kutumia CSR kusaidia ujenzi wa miradi ya maendeleo kijijini humo.

Kwa upande wake Meneja wa Mgodi huo,Mhandisi Peter Moha amesema shirika hilo lilianzishwa mwaka 1972 likiwa na jukumu la kuendeleza rasilimali za madini nchini kwa niaba ya serikali.

Amesema Shirika hilo lilifanyiwa maboresho mwaka 2015 kupitia Public Corporative (Establishment) (Amendment ) Order 2015 yaliyolenga kushirikiana kuwa chombo madhubuti cha kuwekeza katika sekta ya madini kupitia mradi wa kimkakati (Mining Strategic Projects) ili kuongeza pato la Taifa.


Anasema mgodi wa makaa ya mawe Kiwira -Kabulo uliopo Kijiji cha Kapeta Kata ya Ikinga wilayani Ileje mkoani hapa unaendeshwa na STAMICO na ni Mgodi wa chini ya ardhi (Undeground) una ukubwa wa kilometa 8.7 ulifunguliwa rasmi mwaka 1988.

Ambapo ameeleza kuwa baada ya kufanyiwa utafiti na kampuni ya kichina mwaka 1988 ulionesha kuwa na Reserve ya tani milioni 80.6,ukiwa chini ya ubia mwaka 2008 tani milioni 2 zilichimbwa na makaa hayo yalikuwa yakihudumia viwanda vya ndani ikiwemo Mbeya Cement.

Anaesema mwaka 2014 shirika lilikabidhiwa mgodi na kufanya juhudi za kufufu na kuboresha maeneo mbalimbali yaliyokuwa kwenye mnyororo wa uchimbaji kwa kutumia milioni 481.250,kununua na kufunga mtambo unaozalisha mitambo ya kutengeneza makaa mbadala kwa matumizi ya nyumbani kwa kiasi cha bilioni 3.9(3,996,080,000).

Hata hivyo amesema shirika limepanga kuzalisha zaidi ya tani 100,000 na ndiyo maana wamenunua mizani mitatu ya kisasa ya milioni 160 na baada ya ukarabati huo wameweza kuuza makaa ya mawe kwa bilioni 1,22 ndani ya mwezi mmoja.

Anasema mpango wa muda mrefu ni kuanzia 2024/2025 wamepanga kuzalisha zaidi ya tani 600,000 za makaa ya mawe kwa mwaka,huku kiasi kinachotarajiwa kukusanywa kwa mwezi ni bilioni 4.147 kwa sasa wapo katika usimikaji wa mtambo mkubwa.

Baadhi ya wananchi akiwemo Staford Kayange,amesema serikali imefanya kazi nzuri kufufua mgodi huo hali itakayoongeza fusa za ajira huku akiomba wafanyakazi wa zamani walipwe madeni yao ya awali ambayo ni zaidi ya bilioni 1.

Baada ya mwananchi huyo kuzungumza dai hilo Mratibu wa Mgodi huo Peter Moha anasema tayari uhakiki ulifanyika na malipo hayo yatalipwa na hazina hivyo wananchi wawe watulivu wakati serikali ikiwa katika harakati za mwisho kulipa fedha hizo.