October 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

STAMICO kinara wa mageuzi,Rais Samia aimwagia sifa

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan
amelipongeza Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa mageuzi makubwa
ya kiutendaji yaliyopelekea Shirika kuendesha miradi yake kwa faida
kubwa.

Dkt.Samia alisema hayo jana wakati akihutubia katika Kikao Kazi cha
Watendaji Wakuu na Wenyeviti wa Bodi wa Taasisi za Umma kinachoendelea
mkoani Arusha.

Dkt. Samia alisema kuwa, STAMICO imefanya mageuzi makubwa yenye
faida kwa Serikali ambapo katika Mwaka wa Fedha 2018\2019 STAMICO
iliweza kukusanya sh.bilioni 1 na baada ya Serikali kupitia Msajili wa Hazina kuliwezesha Shirika sasa linafanya mageuzi makubwa katika sekta ya madini nchini.

Rais Dkt.Samia alieleza kuwa, mchango wa wachimbaji wadogo kwenye mnyororo mzima wa sekta ya madini umefikia asilimia 40 hii ni kutokana na usimamizi mzuri wa
STAMICO.

Akielezea kuhusu gawio kwa Serikali , Dkt.Samia ameipongeza STAMICO
kwa kutoa gawio la shilingi bilioni 9 kuanzia kipindi cha Mwaka wa Fedha
2018\19 hadi 2023\2024. Naye , Msajili wa Hazina Tanzania
Nehemia Mchechu amesema Sheria mpya inatungwa ili kusimamia Mashirika na Taasisi za umma katika kukuza ufanisi na uwajibikaji ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Dkt.
Samia Hassan.

Kwa upande , Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais ,Mipango na Uwekezaji
Profesa Kitila Mkumbo amesema Rais Dkt.Samia amefungua nchi katika
fursa za kiuchumi na kidiplomasia hivyo ameyataka mashirika ya umma
kutumia fursa hiyo kuimarisha na kufungua uwekezaji ndani na nje ya
nchi.

Sambamba na pongezi hizo , STAMICO imepewa tuzo ya Ufanisi Katika Utendaji kutoka kwa Msajili wa Hazina inayotambua Mashirika ya Umma yanayojiendesha kibiashara kwa faida ambayo yameondokana na utegemezi kutoka Serikali kuu STAMICO imepokea tuzo hii kutoka kwa Msajili wa Hazina kwa mara ya pili mfululizo tangu mwaka 2023 ambapo ilipata tuzo mbili ikiwemo Tuzo ya mashirika yaliyofanya mabadiliko makubwa ya kiutendaji na yenye tija pamoja na tunzo ya mashirika ya umma ambayo yametoa Gawio
kwenye mfuko wa Serikali 2023.