Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.
SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) na Kampuni ya ABSA wametiliana saini mkataba wa mauziano makaa ya mawe ambapo tani 60,000 zitauzwa kwa mwezi kwa wawekezaji hao kwa kipindi cha miaka mitano.
Akishuhudia utiaji saini huo Naibu Waziri wa Madini, Dkt.Steven Kiruswa,jijini hapa leo katika hafla fupi ya utiaji saini mkataba huo Dkt.Kiruswa amesema, STAMICO itakusanya mapato wastani wa shilingi bilioni 4.16 kwa mwezi sawa na wastani wa shilingi bilioni 50 kwa mwaka.
“Niwapongeze Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt.Venance Mwasse na Menejimenti yake kwa kuwa wabunifu katika kutafuta masoko nje ya nchi lakini pia naishukuru STAMICO kwa maamuzi ya kukubaliana na Kampuni ya ABSA katika kufanya biashara nchini kwa sababu pia itatoa ajira zisizo za moja kwa moja 600 na fursa nyingine za ajira kwa Watanzania katika mradi huu,”amepongeza Dkt.Kiruswa.
Nakuongeza,”Ni matumaini yangu kuwa makubaliano haya yaliyosainiwa yatakuwa na manufaa kwa pande zote mbili,”amesema.
Dkt. Kiruswa amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kuendelelea kuifungua nchi ili wawekezaji waweze kuja kuwekeza Tanzania huku akitaja mafanikio ya STAMICO,ambapo amesema katika kipindi cha Julai, 2021 hadi Machi mwaka huu, katika mradi wa Kabulo, tani 17,324 za makaa ya mawe zilichimbwa ambapo tani 12,792 zenye thamani ya shilingi 1.2 ziliuzwa na kulipa serikalini shilingi 174,191,290.87 ikiwa ni mrabaha na ada ya ukaguzi.
“Niwahakikishie wawekezaji wetu wa makaa ya mawe kuwa Tanzania ni nchi salama, inayojali wawekezaji na inayozingatia sheria mbalimbali za nchi na kimataifa na Wizara itahakikisha inafuatilia mwenendo mzima wa mkataba huu ili kupata matokeo chanya kwa Shirika na Kampuni ya ABSA,” amesema.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse amesema, tukio hilo ni matokeo ya mkakati wa kuanza uchimbaji mkubwa wa makaa ya mawe, (mass coal mining).
Huku akisema maandalizi yamekamilika katika ukarabati wa miundombinu ya barabara, daraja na mgodi wa chini ambapo uchimbaji umeanza.
“STAMICO imesaini mkataba mkubwa wakihistoria ndani ambapo STAMICO itauza tani 60,000 kwa mwezi za makaa ya mawe,mkataba huu ni wa kipindi cha miaka mitano, thamani ya mkataba huu ni dola za Marekani milioni 108 na zaidi, sawa na shilingi bilioni 250 za kitanzania kwa miaka mitano,”amesema.
Kwa upande wake Rais wa Kampuni ya ABSA, Bw.Gerges Schmickrath akizungumza katika hafla hiyo ameishukuru wizara kupitia STAMICO kwa kuaminiwa kuwekeza katika mradi wa makaa ya mawe ambapo amesema, mradi huo utakuwa na manufaa kwa watanzania kwa kuongeza pato la Taifa.
More Stories
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja
Gavu aanika miradi iliyotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita Geita
RC Makongoro: Samia aungwe mkono nishati safi ya kupikia