Na Joyce Kasiki,timesmajira, online Chamwino
SPIKA wa Bunge Job Ndugai, amewataka wagombea ubunge na udiwani nchini kuondoa dhana kwamba nafasi hizo ni fursa ya kutengeneza utajiri na badala yake wajiandae kuwatumikia na kuwaletea wananchi maendeleo.
Ndugai ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni mgombea ubunge Jimbo la Kongwa mkoani Dodoma, ametoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa kampeni za Jimbo za Chamwino.
Amesema mawazo ya kufikiria utajiri katika nafasi hizo ndiyo yanawafanya wengi wakipata nafasi hizo kufikiria posho na mwisho wa siku kushindwa kuwatumikia wananchi.
“Naomba niwaambie ninyi wagombea ubunge na udiwani, kama kuna mtu anafikiria anaenda kupata utajiri kwenye nafasi hizi anafikiri vibaya, nafasi hizi ni kwa ajili ya kuwatumikia wananchi,” alisema na kuongeza;
“Ushahidi wa hiki ninachokiongea ninao, wapo watu wengi ambao walishakuwa wabunge, lakini ukiwaona sasa hivi hawana utajiri wowote.”Alisema.
Amesema wakipata nafasi hizo watenga asilimia 40 ya bajeti zao kwa ajili ya maendeleo ya wananchi pamoja na asilimia 10 kwa ajili ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili wajikwamue kiuchumi.
“Miaka ya nyuma Chamwino mlikuwa mnaitia aibu katika hii asilimia 10 mlishindwa kutoa hata asilimia mbili tu kwa ajili ya makundi haya, ninyi mkipata ridhaa mkatenge asilimia 40 ya maendeleo na asilimia 10 ya akina mama, vijana na wenye ulemavu mkimaliza hayo ndio muangalie posho zenu,” amesisitiza
Alitumia fursa hiyo kuwaombea kura wagombea wote wa CCM kuanzia diwani, Mbunge mpaka Rais kwa ajili ya maendeleo ya wana Chamwino na Taifa kwa ujumla.
More Stories
Bodaboda wamchangia Rais Samia Mil 1 ya fomu ya Urais
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani