November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Spika Dkt.Tulia awataka wananchi kuishauri na kuiunga mkono Serikali

Na Esther Macha , Timesmajira, Online,Mbeya

SPIKA wa Bunge na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini,Dkt.Tulia Ackson amesema kuwa serikali inapofanya jambo ambalo si sawa wananchi wanatakiwa kuishauri na waunge mkono sababu lengo ni kuleta maendeleo.

Amesema kuwa wakisema wao ndio wataalamu wa kupinga kuna watu sababu ya kupinga kwao huwa wanaitwa wapinzani sasa wao wanataka kuwa mpinzani kwa hoja ipi.

Dkt.Tulia amesema hayo wakati alipofanya ziara ya kikazi katika shule ya msingi Nero,Samora Sekondari pamoja na shule ya msingi Mwenge zilizopo mkoani Mbeya.

Aidha Dkt.Tulia amesema kuwa serikali inatafuta wawekezaji ili changamoto wanazopitia wananchi ziondoke ili kuweza kufika hatua hiyo lazima serikali ifanye uwekezaji na kutafuta uwekezaji wapo watu serikali inapochukua hatua wao hukaa sehemu na kuhakikisha serikali haipigi hatua kwenye kutafuta maendeleo.

“Lazima sisi wananchi tuishauri serikali,lakini serikali inapofanya maamuzi tuiunge mkono kwasababu tunataka maendeleo ,sasa kuna watu huko ohoo nchi imeuzwa mara bandari imeuzwa kwa shilingi ngapi kama hawana uwezo wa kukujibu waambie na mimi ni sehemu ya watanzania,”amesema Dkt.Tulia.

Hata hivyo Dkt.Tulia amewataka wana Mbeya kutoiga mkumbo kama msafara wa nyumbu ,serikali iletee fedha za barabara ili tuepuke vumbi,niwatoe hofu serikali ipo makini inafuatilia kila hatua na Mbunge wenu amesoma mkataba wote.

Katika hatua nyingine Spika wa Bunge huyo amekabidhi msaada wa mifuko 70 ya saruji na bati bando moja kwa shule ya msingi Nero ili ziweze kusaidia kuezeka darasa moja katika shule hiyo.

Akitoa taarifa ya shule mbele ya Spika Mwalimu Mkuu wa shule ya Nero Suma Lwena amemshukuru Spika kwa namna anavyoipigania shule hiyo.

“Pamoja na ujenzi wa madarasa hayo shule bado inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa madarasa kutokana na uchakavu wa madarasa pia ongezeko la wanafunzi,”amesema Mwalimu Lwena.