December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Spika aagiza ukamilishaji jengo la mama na mtoto

Na Esther Macha, Timesmajira, Online Mbeya

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini, Dkt. Tulia Ackson ameagiza uongozi wa hospitali Rufaa kitengo cha wazazi Meta kuongeza kasi ya ujenzi mradi wa jengo la mama na mtoto ili kupunguza msongamano wa wakinamama wajawazito katika wodi za wazazi.

Dkt Tulia amesema leo Desemba 14, 2022 mara baada ya kushiriki zoezi la kufanya usafi katika viunga vya Hospitali ya Wazazi Meta Mkoani Mbeya Pamoja na kupanda miti akiwa ameambatana na baadhi ya Wananchi wa Jiji la Mbeya.

” Mradi huu umegharimu zaidi ya sh 11 bilioni ambao una uwezo wa kulazwa wagonjwa 200 kwa siku na hivyo kuchelewa kukamilika kunasababisha msongamano wa wagonjwa kutokana na ufinyu wa vitanda na miundombinu ya majengo ” amesema.

Aidha Dkt. Tulia Ackson ambaye pia amewatembelea wagonjwa na wazazi katika Hospitali hiyo ambapo ametoa msaada wa mahitaji mbalimbali ikiwemo sukari, sabuni, mafuta na pampas kwa wagonjwa na wahitaji zaidi ya 170.

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini, Dkt. Tulia Ackson akizungumza na mgonjwa wa Hospitali ya Wazazi Meta mkoani humo.

Akikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo jipya llinalojengwa katika hospitali hiyo, Dkt. Tulia ameipongeza Serikali kwa kutoa fedha za ujenzi huo na pia ameiomba kukamilisha maeneo machache yaliyosalia ili huduma zianze kutolewa rasmi

“Nitoe rai kwa wajenzi kukamilisha jengo hususani mfumo wa maji taka ili vifaa viwekwe na Wananchi wanufaike na huduma hii nzuri inayotolewa na Serikali yao ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan” amesema Dkt. Tulia

Jumla ya Hospitali, vituo vya afya na zahanati 11 zimefikiwa na zoezi la upandaji miti ambapo Spika ametaka zoezi hilo kuwa endelevu kwa kushirikisha kila Mwananchi kuanzia ngazi ya Kata, Wilaya hadi Taifa.

Kaimu Mkurugenzi Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya kitengo cha wazazi Meta, Petro Seme amesema jengo likikamilika litahudumia wagonjwa zaidi ya 200 ambao watalazwa kwa siku.

Seme amesema licha kuwepo kwa changamoto zilizopo lakini bado wapo mstari wa mbele kuhudumia wagonjwa katika hospitali hiyo.

Hadija Yusuph ni mkazi Isanga ambaye amefanyiwa upasuaji katika hospitali amesema kuwa huduma zinazotolewa na watalaam zinawapa matumaini wanawake wajawazito.

“Tunaopata tiba hapa si wana Mbeya tu bali hata mikoa mingine ya jirani tunamshukuru sana Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kujali afya za wanawake kwani tunaamini jengo litakapokamilika litakuwa Neema kwa sisi wanawake maana hatutabanana tena humu wodini” amesema mwanamke huyo.