January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Soko la sabuni lazidi kupaa nchini Tanzania

Na Jackline Martin;

Kufuatia maadhimisho ya wiki ya huduma za fedha kitaifa Mkurugenzi wa Masoko kutoka kampuni ya Cosira inayojishughulisha na uzalishaji wa bidhaa za sabuni Dkt. silverius Komba alisema ushindani katika soko la biashara ni mkubwa hasa katika soko hilo la sabuni.

Akizungumza na Gazeti letu la Majira Mkurugenzi huyo alisema upatikanaji wa mafuta ya kutengenezea sabuni za kuogea na kuoshea vyombo umekua mgumu lakini pia bei zimepanda;

“Changamoto kubwa katika biashara yetu ni upatikanaji wa mafuta ya kutengenezea sabuni lakini kwa vitu vingine tunavyotengenezea sabuni tunapata hivyo mafuta hayo tunapata kutoka Mbeya, mbali na hayo kipindi hiki bei imepanda sana na wale wanaozalisha hawazalishi kama vile mwanzo na sisi tumeamua kulitatua hilo kwa kuweza kupanda michikichi”

Aidha Dkt. Komba alisema utofauti wa bidhaa zao na bidhaa za kampuni nyingine ni mkubwa kutokana na kuzingatia ubora hivyo kupelekea kufanya biashara kwa uhuru;

“Utofauti wa bidhaa zetu ukilinganisha na wengine ni zimerasimishwa kwa maana kwamba Zina alama za TBS, BARCODE, TFDA na tupo karibu sana na TRA hivyo tunafanya biashara kwa kujiamini na uhuru”

Mbali na hayo Dkt. Komba alisema Sabuni hizo zinatengenezwa kwa malengo kwa mfano sabuni ya mche inalenga sana kuimarisha ngozi yaani vitu wanavyotumia kutengenezea sabuni vinalenga kuimarisha ngozi na kufanya ngozi iwe laini na Bora zaidi ambapo huepuka kutotumia kemikali ambapo wanatumia hasa vitu asilia.

Aliongeza kuwa Sabuni ya kuoshea vyombo material yake ni kama ya kwenye sabuni ya kuogea isipokuwa tu kwa aina fulani wanatumia kwaajili ya kuoshea vyombo hivyo inasaidia sana kusafisha vyombo ambapo Zina povu sana na zinadumu kwa muda mrefu.

Pia Dkt. Komba alisema bidhaa hizo za sabuni zimetengenezwa kwa kuzingatia ubora na bei itakayomfanya kila mtu aweze kununua;

“Bidhaa zetu ni sabuni za Miche na sabuni za kuoshea vyombo ambapo bei zake ni; sabuni za kuogea mche mmoja ni shilingi 2500 na kopo 1 la sabuni za kuoshea vyombo 3000”

Dkt. Komba alisema bidhaa hizo zinapatikana kimara baruti lakini kwa wanaohitaji kusafirishiwa au kupata elimu juu ya utengenezaji wa bidhaa hizo pia wanapatiwa muda wowote”