Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
SERIKALI imeagizwa kuharakisha malipo ya mkandarasi wa mradi wa kimkakati wa soko la Jiji la Mwanza likamilike ili wananchi wapate huduma na halmashauri ipate mapato.
Ambapo likikamilika watakusanya bilioni 3.5 kwa mwaka,hivyo serikali iharakishe malipo ya mkandarasi na fedha zikiletwa zisimamiwe ukamilike kwa kumalizia kazi iliyobaki ulete manufaa na tija kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Michael Masanja “Smart’,baada ya Kamati ya Siasa kukagua mradi huo unaogharimu zaidi ya bilioni 23 ambapo kuchelewa kukamilika kwa soko hilo kutasababisha mapato ya Jiji kuwa chini.
Kamati hiyo iliagiza uongozi wa Jiji wakati wa kugawa maeneo ya kufanyia biashara wawape kipaumbele zaidi wafanyabiashara waliokuwa katika soko hilo awali kabla ya kuvunjwa na kujengwa jipya.
Awali Kaimu Mkurugenzi wa Jiji,Erick Mvati amesema mradi huo unaogharimu bilioni 23.367 utaongeza mapato ya halmashauri na kupunguza utegemezi wa serikali kuu ukikamilika kwa mwaka utaingiza bilioni 3.5.
Amesema mradi ambao umefikia asilimia 94.5 umesimama kutokana na malipo ya mkandarasi kuchelewa zaidi ya sh.bilioni 3.6 ambapo ameshalipwa bilioni 18.9 za kazi alizofanya.
Kwa mujibu wa Mvati soko hilo litapunguza msongamano wa machinga barabarani,litakuwa na maduka makubwa na madogo, vizimba vya wafanyabiashara,mama lishe,maegesho ya magari, vibanda vya matunda na nafaka.
Naibu Meya wa Jiji,Bhiku Kotecha amesema watausimami mradi huo wenye manufaa makubwa kwa jamii ili wananchi wafaidi matunda ya kodi zao.
Pia Kamati hiyo ya Siasa ilikagua na kuridhishwa na upanuzi na uboreshaji wa Bandari ya Mwanza Kaskazini pamoja na ujenzi wa jengo la abiria na mizigo.
Kaimu Meneja wa TPA Kanda ya Ziwa,Fransisco Mwanga, amesema mradi huo unagharimu bilioni 18.6 ukiwemo uboreshaji wa mto Mirongo,watahakikisha inakamilika kwa wakati na wamejipanga kutekeleza miradi mbalimbali kwa kuzingati Dira ya Taifa na Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba