January 6, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

SMZ yaendelea na ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na ujenzi wa miradi mbali mbali ya Maendeleo ili kuwapatia huduma bora wananchi wake.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla ameyasema hayo wakati akiwasalimia Waumini wa Masjid Saalim Sogea Mkoa wa Mjini Magharibi alipojumuika nao katika Ibada ya Sala ya Ijumaa.

Amesema Serikali imetenga fedha za Miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Masoko, Skuli, Hospitali za kisasa na Miundombinu hivyo ni wajibu wa wananchi kuunga mkono juhudi hizo kwa kila hali ili Miradi hiyo ikamilike kwa ubora na kwa wakati.

Alhajj Hemed ameendelea kuwakumbusha wazazi na walezi kusimamia malezi ya watoto wao yanayozingatia misingi ya Dini ili kupata jamii yenye maadili mema na hofu na Mungu.

Aidha amekemea tabia ya baadhi ya wazazi kuwapa uhuru uliopita mipaka watoto wao jambo ambalo linapelekea kuwa na jamii inayoiga tamaduni za Mataifa mengine zinazoenda kinyume na Maadili ya Kizanzibari.

Sambamba na hayo Alhajj Hemed amewakumbusha waumini wenye uwezo kufanya haraka kutekeleza Ibada ya Hijja ili kuondokana na dhima waliokuwa nayo mbele ya Allah.

Akitoa Khutba katika Sala ya Ijumaa Ustadh Saleh Ali kutoka Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar ameeleza kuwa waumini waliopewa uwezo wa kutekeleza Ibada ya Hijja tayari wameshaanza kuwasili katika Miji mitakatafu ya Makkah na Madinah ambapo wanajiandaa na kutekeleza Ibada hiyo ambayo ni nguzo ya tano katika nguzo za kiislamu.

Aidha Ustadh Saleh amewakumbusha waumini kuzitumia siku kumi tukufu za dhulhijja kwa kukithirisha Ibada ikiwemo Funga, kusoma Qur’an, Sala za Sunna na kutoa Sadaka ili kuwa karibu na Allah Mtukufu.