Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameahidi kutoa majengo ya ofisi pamoja na usafiri wa bajaji kwa watoa huduma za msaada wa kisheria Zanzibar ili kuwawezesha kuwafikia wananchi wengi wanaohitaji huduma hiyo.
Rais Mwinyi ametoa kauli hiyo leo wakati wa kilele cha maadhimisho ya nne ya wiki ya msaada wa kisheria yaliyofanyika katika ukumbi wa Idrissa Abdul Wakili, Kikwajuni, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.Rais Mwinyi amesema serikali yake inakwenda kuchukua hatua hiyo haraka kutokana na ukweli kuwa huduma za msaada wa kisheria ni kiungo muhimu cha upatikanaji wa haki nchini hasa kwa wananchi wasio na uwezo wa fedha pindi wanapohitaji msaada wa kisheria.
“Nimeelezwa kuwa wasaidizi wa kisheria wanahitaji majengo ya ofisi kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli zao vizuri. Lakini pia wanaomba usafiri wa bajaji, hawa watu hawana makubwa pengine wangetaka kuomba magari. Hivyo mie nalichukua na serikali inakwenda kulishughulikia haraka. Najua tuna mambo mengi lakini ni muhimu sana kwa ajili ya kujenga mazingira bora ya wao kutekeleza majukumu yao.” ameagiza Rais Dkt. Mwinyi.
Saleh Mussa Alawi, ambaye aliwasilisha hotuba fupi kwa niaba ya wasaidizi wa kisheria amesema kuwa wasaidizi wa kisheria walio wengi visiwani humo hawana mejengo binafsi ya ofisi pamoja na usafiri kuweza kuwafikia watu mbalimbali katika jamii ambao wanahitaji huduma za msaada wa kisheria.
“Hatua ya Mheshimiwa Rais kukubali ombi letu ni hatua muhimu katika kuendelea kujenga mazingira bora na endelevu katika sekta ya msaada wa kisheria. Huduma tunazozitoa katika jamii ni muhimu, hivyo ofisi na usafiri vitakwenda kuongeza ufanisi wa shughuli zetu zaidi,” amesema Alawi.
Nae Mjumbe wa Bodi ya Shirika la Legal Services Facility (LSF), Jaji Mstaafu Robert Makaramba awali wakati akiwasilisha hotuba yake amesema ushirikiano kati ya serikali na wadau wa sekta ya msaada wa kisheria ikiwemo wasaidizi wa kisheria ni nyenzo muhimu ya kujenga mazingira mazuri ya wasaidizi wa kisheria na sekta kwa ujumla.
“Suala hili linaanza na uboreshaji wa mifumo, miundo, sera na sheria zitakazohakikisha huduma za msaada wa kisheria zinatolewa katika hali endelevu kupitia uwezeshaji wa serikali kwa kushirikiana na watoa msaada wa kisheria pamoja na wadau wengine,” amesema Jaji mstaafu Robert Makaramba.
Maadhimisho ya wiki ya msaada wa kisheria Zanzibar 2023 yametamatika leo 22 Julai 2023, ambapo pamoja na mambo mengine Rais Dkt. Mwinyi alihitimisha kwa kukabidhi tuzo kwa wasaidizi wa kisheria ambao wamekuwa mstari wa mbele kutoa huduma za msaada wa kisheria katika jamii kwenye masuala mbalimbali ikiwemo eneo la haki za binadamu, watu wenye changamoto ya ulemavu, mazingira na ardhi.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa