November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

SMZ kudhibiti mfumuko wa bei ya mafuta na bidhaa nyingine

Na Mwandishi wetu,timesmajira,online  

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua za makusudi kudhibiti tatizo la mfumuko wa bei ya mafuta na bidhaa mbalimbali ili kupunguzia makali wananchi visiwani humo.

Akizungumza hayo leo alipokuwa kwenye mkutano na viongozi wa madhehebu ya dini ya Kikristo Zanzibar,mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Amani Utengamano Welezo mkoa wa mjini Magharibi Unguja ambao umewakutanisha viongozi mbalimbali wa dini ya Kikristo Zanzibar.

Amesema hivi karibuni imetangaza serikali itatoa ruzuku kwenye mafuta ili kuzuia kupanda kwa bei.

“Mafuta yalikuwa yamefikia Sh. 2461 tumerudisha sasa mpaka 2300 lengo tufanye hivyo hivyo upande wa chakula ili wananchi waweze kumudu Maisha ya kila siku,”Amesema

Rais Mwinyi amesema ameendelea kutilia mkazo suala la kudumisha amani na mshikamano miongoni mwa jamii za wazanzibar.

Amesema Serikali itaendelea kutoa huduma kwa wananchi wote pasipo kujali dini wala dhehebu kama katiba inavyoelekeza.

“Nawapongeza na kuwashukuru viongozi wa dini kwa kuendelea kutoa mchango mkubwa jamii katika huduma mbalimbaliza kijamii,”Amesema

Kwa Upande wake  wa Baraza la Maaskofu Zanzibar,Mchungaji Shukuru Maloda amesema wakristo wa Zanzibar wanaunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Rais Mwinyi katika kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani na utulivu ili kufanikisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Zanzibar,Agostino Shao aliomba Serikali kuweka mawakili wa kushughulikia kesi za udhalilishaji tangu hatua za mwanzo za upelelezi wa kesi hizo,ikiwa ni hatua ya kuziba mianya kwa jamii kufanya usuluhishi au kuingiza muhali na kuvuruga mustakabali wa kesi hizo.