Na Hadija Bagasha,TimesMajira Online- Handeni
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge maalumu wa Uhuru Kitaifa 2021, Luteni Josephine Mwambashi amesema Mkoa wa Tanga umebarikiwa ardhi inayokubali kilimo cha aina yeyote, hivyo hawategemei kukuta mtoto anapata tatizo la utapiamlo.
Awali akizungumza mara baada ya mwenge wa uhuru kuwasili wilayani humo, Mkulima wa shamba la Mihogo lenye ekari 10 ambapo kiongozi huyo alionyesha kufurahishwa na kilimo hicho.
Luteni Mwambashi amesema kuwa, katika maeneo yote ya Mkoa wa Tanga mwenge wa uhuru ulipopita kwa ajili ya kukagua, kuzindua na kuweka jiwe la msingi umebaini kuwa ardhi ya mkoa huo inakubali kilimo cha aina yeyote.
Hivyo amesema hategemei kuona wala kusikia tatizo la utapiamlo linawapata watoto, hivyo amehimiza viongozi idara ya kilimo kuhamasisha jamii kupanda mazao mbalimbali ambayo pia yatawasaidia kuondoa tatizo la njaa.
“Ardhi ya Mkoa wa Tanga umebarikiwa sana kukubali kilimo chochote jambo kubwa ninalotaka kusema utakuwa ni aibu kuona tatizo la utapiamlo linawapata watoto wetu, “amesisitiza Luteni Mwambashi.
Jumla ya miradi 9 yenye thamani ya shilingi milioni 851.704 imezinduliwa, kukaguliwa na kuwekwa jiwe la msingi wilayani Handeni mkoani Tanga.
Katika miradi hiyo 4 imekaguliwa, 1 umezinduliwa na 4 itawekwa jiwe la msingi ambapo mwenge huo umekimbizwa kwenye kilomita 143, tarafa 4, kata 13, vijiji 19 na mitaa 6.
Katika mchanganuo wa miradi hiyo serikali kuu imetoa milioni 718, Halmashauri milioni 157 huku wananchi wakichangia milioni 75.885.
Ukiwa wilayani Handeni Mwenge maalumu wa uhuru uliipongeza wilaya hiyo kwa namna walivyoweza kujipanga katika mapokezi ya mwenge lakini pia katika miradi yao wameonyesha ufanisi wa kiwango kikubwa kuanzia kwenye maandalizi ya taarifa zao.
Amesema hali hiyo inaonyesha wazi kabisa kuwa viongozi wa wilaya hiyo wamekuwa wakifanya kazi kwa kushirikiana ambapo amesisitiza kuwa waendelee na ushirikiano huo kwa kuwa serikali inataka hivyo ili kuwaletea maendeleo ya haraka wananchi.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba