Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
Kauli hiyo ilitolewa Novemba 16, 2021 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akifungua kongamano la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Uingereza katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu alisema katika kipindi kifupi Rais Samia ameboresha mahusiano na nchi mbalimbali ikiwemo Uingereza, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kukuza uchumi.
Alisema Rais Samia ameongeza usimamizi wa sera za soko huria, sera za kiuchumi na kifedha zenye mwelekeo wa kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Alisema kwa kipindi cha Machi hadi Agosti 2021, Tanzania imeongoza kwa kuvutia kiwango kikubwa zaidi cha uwekezaji kutoka nje kwa ukanda wa Afrika Mashariki ambapo kiwango cha uwekezaji kutoka nje kilifikia Dola za Marekani bilioni 2.9.
Dhamira hiyo ya Rais Samia imezidi kufikiwa kwa kiwango cha kuvunja rekodi ambapo kati ya Julai na Novemba, mwaka huu (2022) Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesajili miradi ya uwekezaji 132 yenye kiwango cha thamani ya USD bilioni 3.16.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, John Mnali alisema wiki hii, kuwa miradi hiyo imeongezeka kwa asilimia 259 ikilinganishwa na thamani ya miradi (USD milioni 881) iliyosajiliwa katika kipindi cha Julai – Novemba 2021.
Mnali alisema sababu za ongezeko kubwa la miradi iliyosajiliwa na TIC linatokana na jitihada za Serikali za kutangaza fursa mbalimbali za Uwekezaji zilizoko hapa nchini kupitia ziara mbalimbali za viongozi wa kitaifa nje ya nchi pamoja na juhudi za Serikali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.
Mtaalamu wa masuala ya uchumi, Anna Paul, akizungumzia mafanikio hayo yaliyopatina, alisema mwaka huu, 2022 Rais Samia amefanikiwa kwa kiwango cha juu kuifungua nchi na kuonekana ni sehemu salama kwa uwekezaji na kuvutia watalii.
Alisema kilichowaletea utulivu wafanyabiasha na wawekezaji wengi kujitokeza kuwekeza nchini ni pamoja na hotuba ya Rais Samia aliyoitoa mwaka 2021 mara baada ya kuwaapisha makatibu wakuu wa wizara mbalimbali na manaibu wao.
Katika hotuba yake hiyo, Rais Samia alisema licha ya Tanzania kutangazwa kuingia kwenye uchumi wa kati, hali ya kiuchumi bado ni ngumu kutokana na wawekezaji wengi kuamua kuhamisha biashara zao katika mataifa mengine kufuatia kile alichokitaja kuwa ni urasimu na unyanyasaji wa baadhi ya watendaji Serikalini.
Rais Samia alisisitiza kuwa Tanzania inawahitaji zaidi wawekezaji kuliko wao wanavyohitaji kuwekaza katika nchi hii.
Rais Samia aliitaka ofisi ya waziri mkuu, kuhakikisha wanaondoa urasimu katika mchakato wa kutolewa kwa vibali vya kazi kwa wawekezaji na kuwataka kuacha mara moja kuwalazimisha wawekezaji kuajiri wafanyakazi wa kitanzania kwani wanao uhuru wa kuchagua wa kufanya nao kazi.
Paul alisema mwaka 2022 Serikali ya awamu ya sita imefanikiwa kuifungua nchi hasa kwa kukaribisha wawekezaji, jambo ambalo linakaribisha mitaji.
“Juzi nimewasikia TIC wakisema wamesajili miradi ya uwekezaji ya dola bilioni 3.16, hili sio jambo dogo ndani ya miezi mitano, sasa hivi badala ya wawekezaji kutukimbia, wanamiminika nchini,” alisema Paul na kuongeza kwamba Rais Samia anastahili pongezi kwa hilo.
“Ukiifungua nchi, umefungua mitaji na wawekezaji katika eneo fulani, mfano Royal Tour. Ukikuza utalii unakuza ulaji wa vyakula mbalimbali vya ndani pamoja na kuongeza fedha za kigeni,” alisema
Alisema mwaka 2020 Tanzania ilipokea uwekezaji kutoka nje wa Dola za Marekani bilioni moja, lakini kwa Julai na Novemba 2022 imesajiliwa miradi ya uwekezaji yenye thamani ya Dola la Kimarekani bilioni 3.16 na kwamba hayo ni mafanikio makubwa kwa nchi.
“Hili limefanikiwa kutokana na juhudi za makusudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuimarisha mazingira ya uwekezaji,” alisema Paul.
More Stories
Siri ya Rais Samia kutembea kifua mbelea kijivunia Mapinduzi Matukufu ya Z,bar
Rais Samia anavyotimiza ahadi yake ya kumtua ndoo ya maji mwanamke
Rais Samia anavyozidi kusogeza karibu watoto wa kike na kasi ukuaji teknolojia