September 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Singida inavyodhamiria kuwainua wanawake kiuchumi kupitia kilimo cha alizeti

Na John Mapepele,TimesMajira Online.

TANZANIA ni miongoni mwa nchi ambazo Serikali yake chini ya Rais John Magufuli imefanya kazi kubwa ya kuwakomboa wanawake na wasichana dhidi ya ukatili wa kijinsia katika kipindi cha miaka mitano 2015-2020,hali ambayo imeyafanya mataifa na mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa kuunga mkono jitihada hizo kwa vitendo.

Dhamira ya dhati ya kuwathamini wanawake imeonekana wazi ambapo kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania uongozi wa juu wa Serikali kwa nafasi ya Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeshikiliwa na mwanamke,Mama Samia Suluhu Hassan ambaye ameonyesha uwezo mkubwa katika kupeperusha bendera ya Tanzania ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Aidha,katika kipindi hiki,Taifa la Tanzania lilizindua kampeni maalum Kupinga Ukatili wa Kijinsia na kusema kwamba,Serikali imeandaa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto kwa lengo la kupunguza kiwango cha ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika jamii ya kitanzania kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022.

Mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia (2000); Mkakati wa Taifa wa Maendeleo ya Jinsia (2005); Sera ya Maendeleo ya Mtoto (2008); Sheria ya Makosa ya Kujamiiana – SOSPA (1998).

Serikali imekuwa ikisisitiza kuwa utekelezaji wa mpango huo utachangia katika utekelezaji wa mipango na Mikataba ya Kikanda na Kimataifa kuhusu usawa wa kijinsia, uwezeshaji wanawake na wasichana pamoja na haki na ustawi wa mtoto.

Ili kuhakikisha kuwa jambo hili linachukuliwa kwa uzito unaositahili mwaka 2018,Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ilielekeza Wakuu wa Mikoa wote kuhakikisha wanasimamia uanzishwaji wa Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto kama inavyoelekezwa katika Mwongozo wa uratibu wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto sanjari na kutenga bajeti maalum.

Pia Waziri Mkuu aliongeza kuwa watu wenye ulemavu wana mahitaji maalumu na ni wahanga wa ukatili wa kijinsia ameelekeza Jeshi la Polisi kuboresha Dawati lake la jinsia ili liweze kushughulikia kikamilifu masuala ya ukatili wa kijinsia dhidi ya watu wenye ulemavu. Na kuanzia sasa linaitwa Dawati la Polisi la Jinsia, Watoto na Watu wenye Ulemavu.

Kwa Mujibu wa Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa, ukatili wa kijinsia ni hali ya kutenda vitendo viovu, vinavyodhalilisha, vinavyotesa, vinavyonyanyasa, vinavyokandamiza, visivyojali haki za kuishi kwa binadamu anaweza kuwa wa kiume au kike. Ukatili wa kijinsia huja katika taswira nyingi.

“Aidha, kwa uchache tunapozungumzia ukatili wa kijinsia tunamaanisha vitendo kama vile, vipigo, ubakaji, ukeketaji, ulawiti, matusi, lugha na vitendo vya udhalilishaji pamoja na kunyimwa fursa za kushiriki katika shughuli za kiuchumi.”

“Hivyo, ukatili wa kijinsia ni unyanyasaji wowote unaofanywa na mtu dhidi ya mtu mwingine bila kujali umri, maumbile, kabila, rangi, dini au mtazamo wa kisiasa. Unyanyasaji huu unahusisha mambo mengi kama kumpiga mwanamke au mwanamme, kumnyima mtoto elimu, kumlawiti mtoto wa kike au kiume, kumbagua mtu katika mahitaji ya msingi au kuwanyima urithi warithi wanaohusika.

Septemba 29, mwaka huu dunia imeshuhudia Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia usawa na kijinsia na wanawake (UN Women) na Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Idadi ya Watu (UNFPA) kupitia ufadhili wa shirika la KOICA wamezindua mradi wa “Tuufikie usawa wa jinsia kupitia kuwawezesha wanawake na wasichana” utakaogharimu takribani bilioni 11.5 za kitanzania ambao utatekelezwa katika Wilaya ya Ikungi mkoani Singida na Msalala mkoani Shinyanga katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia Oktoba 2020 hadi Septemba 2023.

Akizindua mradi huo kwa niaba ya Serikali ya Tanzania,Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Rehema Nchimbi anasema lengo kuu la mradi huo ni kuwawezesha wanawake na wasichana kuwakwamua kiuchumi na kijamii katika mikoa ya Singida na Shinyanga ili kufikia usawa wa kijinsia ambapo amewataka watendaji wote wa Serikali ambao watatekeleza mradi huo kuwa makini katika utekelezaji wa mradi ili malengo ya mradi huo yaweze kufikiwa.

Anasema Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali watendaji ambao kwa namna moja au nyingine hawataendana na kasi ya utekelezaji wa miradi chini ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli ambapo amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ili kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli.

Dkt.Nchimbi anafafanua kuwa,katika Mkoa wa Singida, mradi huu utanufaisha Wilaya ya Ikungi katika kutekeleza malengo makuu mawili ambayo ni kuwawezesha wanawake na wasichana kiuchumi kupitia zao la alizeti na mbogamboga pia kuimarisha na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuzuia na kutokomeza ukatili wa kijinsia.

Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan akiwa katika ziara yake kwenye Wilaya ya Ikungi Mkoa wa Singida hapo jana anasema kazi nzuri zinazofanywa na Rais John Magufuli katika nyanja mbalimbali ndiyo zinazoyafanya jumuiya za kimataifa kuunga mkono kwa kutoa misaada kupitia miradi mbalimbali hapa nchini.

Anaongeza kuwa Serikali ina dhamira ya dhati ya kuwakomboa wanawamke wa Tanzania kwa kuwainua kiuchumi kwani kwa kwa kuwawezesha wanawake watakuwa wameliwezesha taifa zima kwa ujumla.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa KOICA Tanzania, Jieun Mo, walengwa wasio wa moja kwa moja takribani wakazi 40,000 kutoka kwenye wilaya ya Ikungi na Msalala na walengwa wa moja kwa moja 2350 wanawake na wasichana kutoka katika wilaya hizo watanufaika na mradi huu ambapo pia wanaume na wanawake 6000 wa Wilaya ya Ikungi watanufaika kwenye eneo la muingiliano wa hati za ardhi.

Mo ameainisha kuwa shughuli za mradi katika kuwaweza wanawake kwenye eneo la uchumi zitajikiza zaidi kwenye kuimarisha uwezo wa wanawake na vijana wakulima ili waweze kutumia njia nzuri za kilimo na hali ya hewa katika uzalishaji wa alizeti na kilimo cha bustani, kukuza uuzaji wa pamoja, ujuzi wa ujasiriamali na wakala wa uchumi wa wanawake na kuimarisha usalama wa ardhi na umiliki.

Amesisiza kuwa shughuli hizo zitatekelezeka kupitia kuunda vikundi vya uzalishaji wa kilimo cha bustani kwa wanawake, kuunganisha wanunuzi wa vikundi vya wakulima vya wanawake,kusaidia ujenzi wa ghala kubwa moja la alizeti na kituo cha ukusanyaji kilomo cha bustani ili kuboresha uuzaji wa pamoja na utunzaji baada ya kuvuna, kutoa mafunzo ya ujasiriamali, kutoa mafunzo ya ujasiriamali na ufikiaji wa habari za kifedha na kufuatilia ushauri wa usimamizi wa biashara na fedha na kukuza umiliki wa ardhi pekee na wa pamoja wa wanawake kupitia utoaji wa Hati za Haki za kimila za Makaazi(CCROs).

Mwakilishi wa UN Women Hodan Addou ameishukuru Serikali ya Tanzania kuwa ushirikiano wake katika kuhakikisha kuwa mradi huu hatimaye umeanza kutekelezwa ambapo amesema Shirika lake linaunga mkono juhudi za Serikali za kumkomboa mwanamke ili kuondokana na unyanyasaji wa kijinsia.

Addou amesisitiza kuwa mradi utasaidia uwezeshaji kijamii kwa kuwawezesha wanawake kusimamia haki zao, kujenga ujuzi wa ujasiiamali wa wanawake na wasichana kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia na kuimarisha mifumo ya kuzuia na kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia kupitia kuanzisha na kuandaa vifaa katika madawati matatu ya Polisi ya Jinsia na Watoto.

Pia kuanzisha vituo vitatu vya huduma ya dharura katika vituo vya wilaya, kuunda nafasi salama ya umma, kujenga uwezo wa nambari ya msaada ya watoto kitaifa, kuunda na kuimarisha Klabu za Wasichana na kuunda Kamati za ulinzi na ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania Zlatan Milisic ameipongeza Serikali kwa kuwa na mradi huo na kuongeza kuwa mradi huo unaendana na malengo ya endelevu ya 2030 hususani lengo namba 5 kuhusiana kuwaendeleza wanawake katika nyanja mbalimbali na kuongeza kuwa mwaka 2020 ni mwaka muhimu sana kwa kuwa tunaelekea katika kutimiza miaka 25 ya azimio la wanawake la Beijing.

Anasema kuwa malengo endelevu ya 2030 yameeleza kuwa ili kufikia maendeleo ya nchi kumtambua mwanamke ni jitihada muhimu sana katika kuharakisha na kutimiza malengo yote ya maendeleo ambapo ameihakikishia Serikali ya Tanzania kuendelea kufanya kazi kwa karibu sana ili kuhakikisha wanawake wanakuwa chachu ya maendeleo katika nchi ya Tanzania.

Mwakilishi wa UNFPA, Dkt.Winfred amesema kuwa uzinduzi wa mradi umelenga kutokomeza aina zote za unyanyasaji wa kijinsia na kuimarisha usawa katika jamii ikiwa ni pamoja na kuimarisha maisha ya wanawake ambapo amesisitiza kitovu cha matatizo ya kijinsia ni wanaume na mila na desturi potofu zinazomtazama mwanamke kwa kumdharirisha hivyo juhudi za makusudi zinatakiwa kufanywa za kuwaweka wanaume mbele ili kutokomeza unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake.

Kwa upande wake,Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt.Anjelina Lutambi amesema programu hii ya pamoja kati ya UN Women,UNFPA na Halmashauri ya Ikungi inasaidia juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuoanisha na Mpango wa Maendelea ya Sekta ya Kilimo (ASDP)II, Mpango Mkakati wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (NPA-VAWC 2017/18-2021/22) na Sheria ya Ardhi ya Kijiji, kuendeleza usawa wa kijinsia na kumaliza umasikini kwa kuboresha uwezeshaji wanawake kiuchumi,mabadiliko ya kilimo,kukomesha aina zote za ukatili dhidi ya wanawake na watoto na kuimarisha mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji.