Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema
Mfumo wa Tathmini ya Mahitaji ya Rasilimaliwatu (HR- Assesment) uliojengwa na Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ndani ya kipindi cha miaka minne ya utendaji wa Serikali ya awamu ya sita umebaini upungufu wa watumishi 441,366 katika taasisi za umma.
Amesema Mfumo ulibaini uwepo wa watumishi 597,396 wakati mahitaji ni watumishi 1,036,762 ambayo ni zaidi ya asilimia 73 ya watumishi waliopo.
Simbachawene amesema hayo jijini hapa leo Aprili 17,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita.
“Katika kusimamia Mipango na Uendelezaji Rasilimali watu katika Utumishi wa umma, Serikali kupitia Ofisi hii baada ya kuona kuna tatizo la upungufu wa watumishi katika maeneo mengi, ilitafuta namna bora ya kuondoa changamoto hiyo kwa kujenga Mfumo wa Tathmini ya Mahitaji ya Rasilimaliwatu (HR-Assessment).
“Mfumo huu wa Tathmini ya Mahitaji ya Rasilimaliwatu ni msaada mkubwa kwani unabainisha idadi ya watumishi walioko katika kila kituo cha kazi na upungufu au ziada iliyopo ili kuwa na idadi ya watumishi sahihi katika sehemu sahihi za utekelezaji wa majukumu yao,”amesema Simbachawene.
Ameeleza kuwa Kupitia mfumo huo taasisi za umma zimewezeshwa kuandaa mahitaji ya watumishi ambapo hadi kufikia Mei, 2024 Mfumo umechakata takwimu kwa Mikoa yote 26 ya Tanzania na kuzifikia taasisi 534.
“Baada ya majumuisho ya Taarifa za tathmini ya mahitaji ya watumishi kwa Taasisi hizo ilibainika kuwa watumishi waliopo ni 597,396, mahitaji ni 1,036,762 na hivyo kuwa na upungufu wa 441,366 ambayo ni zaidi ya asilimia 73 ya Watumishi waliopo,”amesema.
Vilevile Simbachawene amesema kuwa Serikali Kupitia Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora ilijenga mfumo wa Usimamizi wa Utendaji Kazi katika Utumishi wa Umma (e-UTENDAJI – PEPMIS/PIPMIS) unaotumika kusimamia utendaji kazi wa watumishi wa umma na taasisi za umma ili kuwezesha kubaini kiwango cha utendaji kazi na uwajibikaji wa viongozi na watumishi wa umma ambapo Watumishi wa Umma 571,586 kati ya 589,076 wameanza kutekeleza mfumo huo.
Pia amezungumzia mfumo wa e-Mrejesho,ambapo amesema Ofisi hiyo imepokea mrejesho jumla ya hoja 146,204, ambapo hoja 144,222 zilishughulikiwa na hoja 1,313 zinaendelea kushughulikiwa kupitia Idara na Vitengo.
“Utaratibu huu umeleta mafanikio makubwa ambapo uwajibikaji umeongezeka kwasababu ya urahisi wa ufuatiliaji kupitia mifumo ya TEHAMA, na wananchi wameongeza imani yao kwa Serikali kutokana na namna wanavyohudumiwa na kupata mrejesho kwa njia rafiki zinazowapunguzia gharama za usafiri kwa ajili ya ufuatiliaji,”amesema.
Katika suala la Ajira mpya Simbachawene amesema katika kupambana na upungufu wa ajira, Serikali kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ilifanikisha mchakato wa Ajira na kuwapangia vituo vya kazi jumla ya waombaji kazi 55,162 huku waombaji kazi waliopangiwa vituo vya kazi wakiongezeka kutoka 7,659 mwaka 2020 hadi 20,158 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 163.19.



More Stories
Dkt.Mpango azindua shule ya sekondari itakayojengwa na CRDB Dar
NBAA, ZIAAT wasaini hati ya makubaliano ya kufanya kazi pamoja
Simbachawene:Tanzania,Afrika inahitaji viongozi wa kimageuzi katika kuhamasisha juhudi za pamoja