March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Simbachawene: Dawa za Covid-19 Zisambazwe Haraka Kwa Wananchi

Simbachawene: Dawa za Covid-19 Zisambazwe Haraka Kwa Wananchi

Na Joyce Kasiki,Dodoma

WAZIRI  wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, ameitaka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kuhakikisha dawa zilizobuniwa kwa ajili ya kinga na tiba ya ugonjwa wa Covid-19 zinasambazwa kwa haraka katika maduka makubwa ya dawa nchini ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Akizungumza katika banda la NIMR kwenye maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma jijini Dodoma, Waziri Simbachawene alisema ni muhimu dawa hizo zipatikane kwa urahisi kwa kuwa zimetokana na tafiti za kisayansi zilizofanyika hapa nchini.

“Ni lazima wananchi wanufaike moja kwa moja na matokeo ya tafiti hizi. Tunataka dawa hizi ziwepo katika maduka yote makubwa ya dawa kote nchini. Si vema zikabaki kwenye maabara au ndani ya taasisi pekee,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Mtafiti Mwandamizi kutoka NIMR, Dkt. Akili Kalinga, alisema taasisi hiyo imepokea agizo hilo kwa uzito na tayari imeanza utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa usambazaji wa dawa hizo.

“Dar es Salaam tayari imeanza kupokea dawa hizi kupitia maduka makubwa ya dawa, na juhudi zinaendelea kuhakikisha mikoa yote nchini inafikiwa,” alisema Dkt. Kalinga.

Aidha, alibainisha kuwa NIMR inaendelea kufanya tafiti mbalimbali kuhusu magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza kama vile kisukari, saratani, kifua kikuu, malaria, pamoja na magonjwa mapya ya mfumo wa upumuaji. Vilevile, taasisi hiyo imeweka mkazo kwenye utafiti wa tiba asilia zinazotokana na mimea ya dawa.

“Tunatambua mchango wa tiba za asili ambazo zilitumika tangu enzi za mababu. Kama taasisi ya utafiti, tunakusanya na kuchambua taarifa za kisayansi kuhusu mimea tiba kwa lengo la kuimarisha mfumo wa afya unaotegemea rasilimali zetu za ndani,” aliongeza.

NIMR ni taasisi chini ya Wizara ya Afya yenye jukumu la kufanya utafiti kuhusu magonjwa mbalimbali ili kusaidia serikali katika kuweka sera bora za afya na kutoa tiba sahihi kulingana na ushahidi wa kisayansi.