Na Mwandishi wetu, Timesmajira
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa George Simbachawene ameipongeza Tume ya Madini kwa kazi kubwa na yenye matokeo chanya katika ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali na kuchochea maendeleo ya Sekta ya Madini nchini.
Akizungumza alipotembelea banda la Tume ya Madini katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma,Simbachawene amesema mafanikio hayo ni matokeo ya uongozi thabiti wa Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde.
“Nawapongeza Tume ya Madini, na nampongeza sana Waziri wenu Anthony Mavunde kwa kusimamia kwa weledi ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali, kufufua migodi iliyokuwa imesimama, pamoja na kutoa ajira kwa vijana. Haya ni mafanikio ya kujivunia,” amesema Simbachawene.
Ameeleza kuwa Sekta ya Madini kwa sasa inachangia zaidi ya asilimia 10 ya Pato la Taifa, jambo linaloonesha mchango mkubwa wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa, huku akitoa wito kwa Tume ya Madini kuongeza juhudi zaidi ili kuvuka lengo la sasa.
Katika hatua nyingine, Waziri Simbachawene amesema kaulimbiu ya Sekta ya Madini inayosema “Madini ni Maisha na Utajiri” siyo kauli ya bahati nasibu, bali ni uthibitisho wa mchango wa sekta hiyo katika kuimarisha maisha ya Watanzania na kuongeza utajiri wa Taifa.
“Hii si kauli ya bahati mbaya. Sekta hii ina mchango wa kweli katika nyanja zote—ajira, biashara, teknolojia, na mapato ya ndani. Tume ya Madini ifanye kazi kwa nguvu zaidi ili Watanzania wote wanufaike na rasilimali zao,” ameongeza.

Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka huu yamejumuisha taasisi mbalimbali za serikali zikiwemo za sekta ya madini, zikionesha mafanikio, huduma, na mipango ya maendeleo kwa wananchi.
Banda la Tume ya Madini limeendelea kuvutia wananchi wengi wanaotaka kupata elimu kuhusu fursa zilizopo kwenye sekta ya madini, hususan kwa wachimbaji wadogo na wajasiriamali wa ndani.
More Stories
REA yaendelea kusambaza Nishati Bora kwa wananchi,yamshukuru Rais Dkt.Samia
Vivo Energy Tanzania, yazindua Kampeni ya “Uliza Oili ya Shell”
Kampeni ya kisheria ya Mama Samia kuondoa migogoro na ukatili