Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.
WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera,Bunge na Uratibu,George Simbachawene ametaja mapambano dhidi ya biashara ya dawa kulevya kama kipaumbele kimoja wapo kati ya vipaumbele vinavyotarajiwa kutekelezwa na ofisi yake kwa mwaka wa fedha wa 2022/23.
Simbachawene ametaja kipaumbele hicho jijini hapa leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa bajeti ya ofisi hiyo baada ya kupitishwa na Bunge katika mwaka wa fedha wa 2022/23.
Amesema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23 Mamlaka ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya Nchini imeidhinishiwa sh.bilion 11.9 kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake.
Ambapo amesema fedha hizo ni ongezeko la asilimia 28.8 ikilinganisha na kiasi cha sh.bilion 8.5 kilichoidhinishwa mwaka wa fedha 2021/22.
Amesema Ofisi itaboresha huduma za tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya kwa kuongeza idadi ya vituo vya tiba na urekebishaji wa tabia ya waathirika wa Dawa za Kulevya nchini pamoja na kuweka programu maalum ya elimu ya maisha na mafunzo ya ufundi.
“Ongezeko hili la bajeti ya mamlaka litaendelea kuimarisha udhibiti wa biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini, kuimarisha ushirikiano miongoni mwa vyombo vinavyojihusisha na udhibiti wa dawa za kulevya kitaifa na kimataifa ikiwa ni pamoja na kubadilishana taarifa pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa taarifa za kiintelijensia zinazohusu biashara haramu ya dawa za kulevya na kuendesha operesheni za pamoja,”amesema.
Waziri huyo pia ametaja vipaumbele vingine kuwa ni Mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi,kujenga uwezo wa kuzuia,kujiandaa na kukabaliana na Maafa kwa Kamati za maafa za ngazi ya mikoa,Halmashauri na
serikali za mitaa pamoja na wadau wengine .
Amesema Ofisi ya Waziri Mkuu iliidhinishiwa na Bunge kiasi cha shilingi bilioni 101 ili iweze kutekeleza majukumu yake katika mwaka wa fedha wa 2022/23.
Hata hivyo amesema Serikali inakwenda kukamilisha mapitio ya sera ya menejimenti ya Maafa ya Mwaka 2004 kwa ajili ya kuboresha mfumo wa uratibu na usimamizi wa maafa nchini pamoja na kuboresha mifumo ya usimamizi wa menejimenti ya Maafa.
Kuhusu mapambano dhidi ya Virusi vya Upungufu wa Kinga Mwilini (UKIMWI) Simbachawene amesema katika kwa mwaka wa fedha 2022/23,Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania iliidhinishiwa na Bunge sh.bilion 14.9
Ameeleza kuwa katika fedha hizo sh.bilion 2.9 ni kwa ajili ya matumizi ya Kawaida na sh.bilion 12 ni kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo.
“Shughuli zitakazotekelezwa kwa mwaka wa fedha 2022/23 ni pamoja na kuratibu upatikanaji wa huduma za VVU na UKIMWI kwenye Mikoa ya kipaumbele ikiwemo Iringa, Kagera, Katavi, Mbeya, Mwanza, Njombe, Pwani, Ruvuma, Shinyanga, Dodoma, Geita, Tabora na Songwe pamoja na kuweka kipaumbele katika kuzuia maambukizi ya VVU kwa vijana wa miaka 15 -24,”amesema.
Hata hivyo amesema ofisi itaendelea kutafuta Vyanzo vya Fedha kwa ajili ya Mfuko wa UKIMWI (ATF) ambao umelenga kuliwezesha Taifa kuwa na rasilimali fedha za kutosha kwa ajili ya kudhibiti UKIMWI hata pale fedha za nje zitakapopungua au kutokuwepo kabisa.
Katika hatua nyingine Simbachawene amesema katika kuhakikisha serikali inaendelea kukuza Demokrasia imeendelea kufanya jitahada mbalimbali zenye lengo la kukuza Demokransia nchini.
Ambapo ametaja jitihada hizo kuwa ni kuhakiki maeneo ya uchaguzi na vituo vya kuandikishia wapiga kwa kuboresha mifumo ya menejimenti ya uchaguzi,kuratibu na kusimamia uendeshaji wa chaguzi ndogo
Pamoja na kuendesha vikao na wadau mbalimbali vikiwemo vyama vya siasa,kutoa elimu ya mpiga kura kwa wananchi,kuimarisha taratibu za upatikanaji na uwekaji wa takwimu kwa kuandaa mfumo maalum, kuboresha sheria za uchaguzi na kuandaa vituo vya kuandikishia wapiga kura.
“Kukamilisha ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Jijini Dodoma ambapo kiasi cha sh.bilion 20.4 kitatumika ambapo ofisi hii itakapokamilika itakuwa na nafasi kwa ajili ya Ofisi kwa Vyama vyote Vya Siasa,
“Kuratibu shughuli za Kikosi Kazi cha Rais Samia Suluhu Hassan cha kuchambua maoni ya wadau wa Demokrasia kuhusu masuala ya Demokrasia ya Vyama vingi vya Siasa nchini,”amesema.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja