January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Simba, Yanga na Azam kukutanishwaTaifa, Rais Dkt. Samia mgeni rasmi

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar

TIMU za Simba, Yanga na Azam zitakutanishwa pamoja kwenye Shindano la Kimataifa la kuhifadhi na kusoma Quran kwa wanawake, linalotajiwa kufanyika katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, Jumamosi ya Agosti 31, 2024, kuanzia asubuhi.

Katika Shindano hilo lililoanzishwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), linatarajiwa kuanza mapema asubuhi ambapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa mgeni rasmi wa shindano hilo litakaloshirikisha wanawake wa nchi 12 duniani.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Msemaji wa Simba, Ahmed Ally, alisema ni furaha kubwa kushiriki katika uhamasishaji wa shindano hilo litakaloshirikisha wanawake wa Tanzania, akiwemo Rais Samia, akiwa kama mgeni rasmi.

“Simba ni timu kubwa barani Afrika, hivyo kualikwa katika shindano hili kusema chochote sambamba na kualika wadau wa michezo wakiwemo wa Simba, ni jambo la kumshukuru Mungu, nikiamini Uwanja wa Taifa Jumamosi utajaa kwa sababu hakutakuwa na viingilio,” Alisema Ally.

Naye Msemaji wa Yanga, Ally Kamwe, aliwataka Watanzania wote wanaofuatilia michezo wakiwemo mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga kuitumia Jumamo kama siku maalum ya kushuhudia neno la Mungu.

“Siku ya Jumamosi Yanga hatutakuwa na ratiba yoyote, hivyo wote wakiwepo wachezaji na viongozi wetu tutajaa katika Uwanja wa Taifa kushuhudia shindano hili lenye maana kubwa katika nchi yetu, ukizingatia kuwa Rais wa nchi, mama yetu Samia atakuwa mgeni rasmi,” Alisema Kamwe.

Msemaji wa Azam FC, Hashimu Ibwe, alisema mpira wa miguu ni mchezo wa furaha, mazoezi na hauhusiani na uadui, ndio maana kwa pamoja wameunganishwa na BAKWATA katika kulisemea shindano la wanawake la kusoma na kuhifadhi Quran, Jumamosi ya Agosti 31.

“Isingekuwa mchezo wa mpira tusingejumuishwa kwa pamoja na viongozi wa dini wakubwa kwa lengo la kufanikisha mashindano haya, ambapo nasi kama Azam tunafurahia kuwepo hapa sambamba na kuguswa na mgeni rasmi, Dkt. Samia siku ya Jumamosi,” Alisema Ibwe.

Kwa mujibu wa BAKWATA, shindano hilo linatambua umuhimu wa michezo, hali iliyowalazimu kuwaalika wasemaji wa vilabu vikubwa vya mpira wa miguu Tanzania, kushiriki katika kuhamasisha wafuasi wao wahudhurie kwa wingi kwenye shindano hilo la Kimataifa.

Mwisho