March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi PPRA akutana na wasanii wa Kombolea,awaeleza fursa za kupata tenda za Serikali 

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Bw. Denis Simba, amekutana na baadhi ya wasanii kutoka kikundi cha sanaa cha Kombolela na kufanya nao mazungumzo kuhusu fursa zilizopo katika mfumo wa manunuzi ya kielektroniki wa serikali ujulikanao kama NeST, pamoja na namna bora ya kushiriki katika zabuni za serikali.

Akizungumza na wasanii hao kwenye banda la PPRA katika Maonyesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea jijini Dar es Salaam, Bw. Simba alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa kipaumbele kwa makundi maalum, ikiwa ni pamoja na vikundi vya sanaa, kwa kutenga asilimia 30 ya zabuni kwa ajili yao.

“Serikali inawatambua wasanii na mchango wao katika jamii. Hii ndiyo sababu sheria ya ununuzi wa umma iliyopitishwa imeweka wazi kuwa taasisi zote nunuzi lazima zitenge asilimia 30 ya zabuni kwa makundi maalum. Tunataka kupitia sanaa yenu, mtoe elimu kwa jamii kuhusu fursa hizi zilizopo kwenye mfumo wa NeST,” alisema Simba.

Kwa mujibu wa Simba, mpaka sasa PPRA imesharatibu utoaji wa zabuni zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 16, huku lengo likiwa ni kufikia utoaji wa zabuni zenye thamani ya hadi trilioni tano.

Wasanii Wapewa Nafasi ya Kuuliza Maswali

Katika kikao hicho, wasanii walipata nafasi ya kuuliza maswali mbalimbali yakiwemo namna ya kusajili kikundi rasmi kinachoweza kushiriki zabuni, jinsi ya kupata mafunzo kuhusu matumizi ya mfumo wa NeST, na masharti yanayopaswa kufuatwa ili kushiriki kwenye tenda za serikali.

Akijibu maswali hayo, Bw. Simba alisema kuwa tayari PPRA imeanza kushirikiana na makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na watu wenye ulemavu wa kuona, kuhakikisha kuwa hakuna kundi linaloachwa nyuma.

“Hatuangalii tu idadi au muundo wa kikundi. Unaweza kuwa na kikundi chenye wanawake asilimia 70, na asilimia iliyobaki mkaweka wanafunzi waliomaliza chuo ambao hawana ajira pamoja na wazee wanaoweza kushiriki kikamilifu. Lengo ni kuwa na vikundi vyenye uwezo na ushirikiano,” alifafanua.

Mfumo wa NeST Ni Lango Kuu

Bw. Simba alisisitiza kuwa mfumo wa NeST ndio njia pekee ya kuomba tenda za serikali kwa sasa. Alieleza kuwa mfumo huo unapatikana mtandaoni, na kinachohitajika ni kuwa na intaneti ili kuweza kuangalia na kushiriki katika zabuni zinazotangazwa.

“Tenda nyingi zinazotangazwa zinaweza kufikiwa kwa urahisi kupitia NeST. Ni mfumo rafiki unaowezesha uwazi na usawa. Huu ni wakati muafaka kwa vikundi kama vyenu kujisajili na kuanza kushiriki,” alisema.

Aliongeza kuwa kuna fursa mbalimbali ambazo vikundi vya sanaa vinaweza kuanza nazo, kama vile utoaji wa huduma za usafi, upandaji wa maua, utunzaji wa mazingira, na hata vifaa vya michezo kwa shule na taasisi.

Mwito wa Kujisajili Rasmi

PPRA imetoa wito kwa vikundi vyote vya sanaa na makundi maalum kujisajili rasmi na kujiandaa kushiriki kikamilifu katika zabuni zinazotangazwa na serikali kupitia mfumo wa NeST. Lengo ni kuhakikisha kuwa fursa hizi zinawanufaisha wananchi wote na kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja kupitia ushiriki wa moja kwa moja kwenye manunuzi ya umma.