Na.Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Mashabiki na wanachama wa timu ya Simba SC tawi la Nyegezi Stendi(Nyegezi Terminal) jijini Mwanza, wametembelea na kutoa msaada wa vitu mbalimbali kwa wafungwa wa Gereza Kuu Butimba lilililopo mkoani humo.
Hii ikiwa ni sehemu ya kusherekea kilele cha siku ya Simba (Simba Day) ,ambayo kwa mwaka huu imeadhimishwa Agosti 6,2023.
Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo Mkuu wa Gereza Kuu Butimba Deogratias Maguza,mbali na kuwapongeza na kuwashukuru mashabiki na wanachama hao,pia ametoa wito kwa mashabiki na wanachama wa timu nyingine kuiga mfano huo kwa kutembelea wafungwa na kuwapa msaada kwani wameonesha uzalendo.
Sanjari na hayo amewaomba wadau wa michezo kutoka vilabu mbalimbali kuwasaidia wafungwa hao jezi na mipira kwani utakapoanza msimu wa Ligi Kuu wa 2023/2024 nao wataanza ligi yao.
“Humu ndani kuna mashabiki wa timu ya Simba SC na timu nyingine waleteeni mipira na jezi ,inapoanza Ligi Kuu na sisi safari hii tunaanza ligi hapa inaitwa Mzee Ramadhan Nyamuka Cup 2023/24 kwani humu kuna wanacheza mpira,timu zote zije hapa kusaidia na kutembelea wafungwa,”amesema Mkuu huyo wa Gereza hilo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Simba SC tawi la Nyegezi Stendi Said Ramadhan, amesema kuwa wakiwa kama wanamichezo wameguswa na kuona katika kusherekea siku ya Simba ni vyema kuwatembelea wafungwa na kuwasaidia kile kidogo walicho nacho.
Said amewaomba wanamichezo na mashabiki wa timu mbalimbali kuwaunga mkono timu zilizopo ndani ya gereza kwa kuwapatia,jezi,mipira na viatu ili kuendeleza vipaji vyao.
“Mchezo ni sehemu ya maisha ya wanadamu naomba wanamichezo wengine tushikamane,tushirikiane na tuwasaidie kwani ndani ya gereza kuna timu zina majina mbalimbali na wanahitaji jezi, mipira,viatu ili waweze kuendeleza vipaji vyao,hivyo wadau tujitokeze ili wapate vifaa hivyo,”.
Mhamasishaji wa Simba SC tawi la Nyegezi Yohana John, amesema kuwa mpira ni kujifunza kwa hatua(step), ukisha jua umemaliza haurudii kujifunza tena hivyo kwa msimu huu wanaatarajia timu yao kufanya vizuri na watashuhudia kushangilia na kuangukiana.
Naye shabiki wa timu ya Yanga SC tawi la Nyegezi Stendi ambaye aliamua kuungana na watani wao wa jadi katika kusherekea Simba Day,Sada Mayombo,amewapongeza mashabiki wa Simba SC tawi la Nyegezi Stendi kusherekea siku yao kwa kuwakumbuka wafungwa.
“Nawapongeza kwa kweli wameonesha uzalendo kwani waliomo ndani ya gereza na sisi tuliopo nje wote ni wa moja,kwani pia wapo mashabiki wa timu mbalimbali,”.
More Stories
Watumishi wa Fahari wafanya Bonanza
Rais Samia atia mkono mchezo wa masumbwi Tanzania
Chino bingwa mpya wa IBA Intercontinental Championship