Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
WAKATI vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) Simba wakihitaji alama tatu muhimu zitakazowasogeza karibu na ubingwa wa msimu huu, wapinzani wao Mbeya City wamesema hawatakubali kudondosha alama tatu ili kujiweka kwenye nafasi salama la kusalia kwenye Ligi msimu ujao.
Timu hizo leo zitakutana katika uwanja wa Benjamin Mkapa huku kila mmoja akitaka kuwa bora kwa mwenzake ili kubadili kile kilichotokea Desemba 13, 2020 baada ya Mbeya City kukubali kichapo cha goli 1-0 katika uwanja wao wa nyumbani wa Sokoine.
Simba ambao wapo nyumbani wanapewa nafasi kubwa zaidi ya kubeba ushindi kutokana na mwendelezo wa matokeo mazuri waliyoyapata msimu huu ambayo yamewawezesha hadi ssa kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi wakiwa na pointi 70 walizopata baada ya kucheza mechi 28 na kushinda 22, sare nne wamepoteza mechi mbili pamoja na kufunga goli 65 huku nyavu zao zikitikishwa mara 11.
Kocha msaidizi wa Simba, Seleman Matola amesema kuwa, wanatambua ugumu watakaokutana nao katika mchezo huo lakini kama timu yenye ki una ubingwa watahakikisha wanashinda mchezo huo ili kubakiza alama tatu kutangazwa kuwa mabingwa wapya wa msimu huu.
Amesema, kama timu wameshakamilisha maandalizi yote na kilichobaki ni wachezaji wao kujitoa na kuonesha kile walichowaelekeza katika dakika 90 za mchezo huo ambao zitaamua nani ataondoka na alama tatu.
Katika mchezo huo, Simba itamkosa kipa wao namba moja, Aishi Manula na Taddeo Lwanga ambao wanatumikia adhabu ya kadi tatu za njano lakini kiungo wao Clatous Chama akiongeza mzuka baada ya kurejea akitokea kwao Zambia baada ya kumaliza mazishi ya mke wake aliyefariki mwanzini mwa mwezi huu.
“Kwa sasa jambo kubwa kwetu ni kuchukua alama tatu katika mchezo huu ambazo zitazidi kutuweka karibu na ubingwa kwani tunachokitaka ni kutangaza mapema ubingwa na hili tutahakikisha linafanikiwa kwani tunapambana kushinda kila mchezo ili kuzidi kujisogeza karibu na ubingwa,” amesema Matola.
Kwa upande wake kocha msaidizi wa Mbeya City, Matezo Wadiba amesema, wataingia katika mchezo huo kwa tahadhari kubwa kwani wanawaheshimu wapinzani wao Simba ambao wamekuwa katika kiwango bora.
Licha ya kulitambua hilo lakini kocha huyo amesema, hawataingia wakiwa wanyonge kwani kwa sasa kitu pekee wanachokihitaji zaidi ni kushinda mechi zao zote zilizosalia ndani ya msimu huu wakianza na mchezo huo dhidi ya Simba.
Wadiba amesema kuwa, kama timu mkakati wao ni kubeba alama tisa ambazo zitawaondoa kabisa kwenye hatari ya kushuka daraja msimu huu na kujihakikishia nafasi yao katika msimu ujao wa Ligi Kuu.
“Tunawaheshimu Simba kwa kuwa ni timu kubwa na inafanya vizuri lakini kusema hivi haimaanishi kuwa tunawaogopa au tutakuwa wanyonge kwani tumejipanga kuja kupambana na tutahakikisha tunakuwa washindani wa kweli na kuwa tutaondoka na alama zote tatu,” amesema kocha huyo.
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania