Na Yusuph Digossi, TimesMajira Online
KIKOSI cha timu ya Simba leo kitakuwa nyumbani kusaka alama tatu muhimu katika mchezo wao wa kiporo namba 116 wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) utakaochezwa kwenye uwanja wa Mkapa dhidi ya timu ya KMC.
Simba itaingia katika mchezo huo huku ikiwatangazia kiama wapinzani wao wakidai ushindi katika mchezo huo utawapa morali kubwa zaidi ya maandalizi kuelekea mechi yao ya kimataifa ya Ligi Mabingwa Afrika watakaoanzia ugenini dhidi ya FC Platinum ya Zimbabwe.
Lakini pia wanataka kuendeleza ushindi baada ya kuchukua alama tatu muhimu katika mchezo wao uliopita kwa kuwafunga goli 1-0 Mbeya City na kukaa katika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi wakiwa na pointi 29 wakiwashusha Azam ambao wapo nafasi ya tatu wakiwa na pointi 28 huku Yanga wakikaa kileleni wakiwa na pointi 37.
Wakati Simba inataka ushindi huo, mipango ya KMC ni kuchukua alama zote tatu ili kumaliza hasira zao za kupoteza mchezo wao uliopita wa ugenini baada ya kufungwa goli 1-0 na Mtibwa Sugar.
Pia wanahitaji kuhitimisha ubabe wa Simba dhidi yao katika mechi za Ligi Kuu kwani katika misimu miwili ya Ligi Kuu iliyopita, KMC ilipoteza mechi zake zote za nyumbani na ugenini.
Katika mchezo wa Desemba 19, 2018 Simba ilishinda goli 2-1, Aprili 25, 2019 Simba wakiwa ugenini walishinda tena goli 2-1, msimu uliopita Simba waliifunga KMC goli 2-0 katika mchezo wa raundi ya kwanza wa Desemba 28 huku Machi Mosi, 2020 wakishinda tena 2-1.
Licha ya ugumu wa mchezo huo unaotabiriwa na wadau wengi wa soka, tayari kocha mkuu wa timu hiyo , Sven Vandenbroeck ameweka wazi kuwa anachikihitaji kwa sasa katika mechi zao ni ushindi utakaowapa morali zaidi kuelekea mechi zijazo ili kushinda na kukaa nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi ili pia kurudi katika mbio za kutetea ubingwa wao kwa msimu wa nne mfululizo.
Akizungumzia mchezo huo, kipa namba moja wa Simba, Aishi Manula amesema kuwa, wanatambua kuwa mchezo huo utakuwa mgumu na wenye upinzani mkubwa lakini malengo waliyonayo ni kupambana na kuchukua alama zote tatu.
Lakini pia mchezo huo utawapa taswira ni namna gani watauendela mchezo wao wa kimataifa dhidi ya Platinum ambao pia wanahitaji ushindi ili kutinga katika hatua ya makundi.
“Tunakwenye kukutana na KMC ambayo tunaifahamu vizuri hivyo jambo kubwa kwetu ni kupambana ili kuweza kubeba alama zote tatu muhimu ambazo zitazidi kutuweka kwenye nafasi nzuri katika msimamo wa Ligi kwani mikakati yetu ni kurudi katika nafasi yetu ya kwanza ambayo mashabiki wameizoea, ” amesema Manula.
Lakini kwa upande wake Ofisa Habari wa KMC, Christina Mwagala amesema kuwa, kikosi chao chini ya kocha mkuu John Simkoko hakina hofu yoyote kuelekea kwenye mchezo huo kwani wanachokwenda kukifanya na kutimza mkakati wao wa kuifunga timu hiyo na kubeba alama zote tatu.
“Hatuna hofu na mchezo wa leo kwa sababu tumejipanga vizuri, tunakikosi imara na wachezaji wazuri ambao wanaweza kupambania alama tatu wanapokutana na timu yoyote, lakini pia tunafahamu kuwa wapinzani wetu wametoka kupata ushindi na sisi tumepoteza hivyo hasira tutazimaliza kwao,”.
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania