January 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Simanjiro yatoa mamilioni ya fedha za mitaji kwa vijana, wanawake, walemavu

Na Mary Margwe, Simanjiro

HALMASHAURI ya Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara imetoa mkopo wa zaidi ya sh.milioni 200 kwa wanawake, vijana na walemavu kutoka katika asilimia 10 ya mapato yake ya ndani ya kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020.

Hayo yamebainisha na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Alfred Myenzi wakati akizungumza na vikundi vya wanawake, vijana na walemavu mbele ya mkuu wa wilaya hiyo, Mhandisi Zephania Chaula kwenye hafla ya kukabidhi mfano wa hundi ya sh. milioni 244,635,557.74.

Myenzi amesema, kwa mwaka wa fedha 2019/ 2020 Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro ilitenga jumla ya sh.milioni 183,414,050.00 ikiwa ni sawa na asilimia 100 ya bajeti iliyotengwa, pamoja na sh.milioni 61,221,507.74 ambayo imetokana na fedha za marejesho ya vikundi.

” Tunaendelea kusisitiza kuwa serikali imetoa mkopo usiokua na riba, jambo ambalo hakuna taasisi yoyote ile ya kifedha inayotoa mikopo bila ya riba isipokua ni serikali pekee, mtaona ni jinsi gani serikali ya awamu ya tano chini ya Mheshimiwa Rais Dkt.John Pombe Magufuli inavyowajali wananchi wake, tuzidi kumuombea Rais wetu afya njema ili aweze kutimiza ndoto alizokusudia katika kuwatumikia wananchi wa Tanzania,”amesema Myenzi.

Aidha, amewataka wanavikundi wote waliopata mikopo hiyo kuhakikisha wanaendelea na marejesho kama utaratibu unavyoeleza, ili wengine nao waweze kupata mikopo hiyo na hatimaye kuweza kuinua uchumi wao.

Akisoma taarifa ya utoaji wa mikopo ya vikundi hivyo kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020 Afisa Maendeleo ya Jamii wa halmashauri hiyo, Asia Ngalisoni alisema,jumla ya vikundi vipatavyo 72 vitanufaika na mkopo huo wenye jumla ya sh.milioni 244,635,557.74 , ambapo utawanufaisha wanachama wapatao 1,412 wakiwemo wanawake 1,075, vijana 332 huku watu wenye ulemavu wakiwa watano.

Ngalisoni amesema, vikundi vya wanawake 51 vimepatiwa sh.milioni 171,635,557.74, vikundi 20 vya vijana wamepatiwa jumla ya sh. milioni 68,000,000 huku kikundi kimoja cha watu wenye ulemavu wakipatiwa sh.milioni tano.

“Mkopo huu umetolewa katika kata zote 18 za wilaya ikiwemo Kata ya Loiborsiret, Laangai, Orkesumet, Terrat, Mirerani, Komolo, Emboreet, Oljoro No.5, Naberera, Endonyogijape, Ngorika, Msitu wa Tembo, Ruvu Remit, Endiamtu, Naisinyai, Laangai na Shambarai,”amesema Ngalisoni.

Aidha, alisema katika kipindi cha mwezi Julai hadi Aprili, 2020 jumla ya sh.milioni 101,737,500.00 zimerejeshwa kutoka katika vikundi mbalimbali vilivyokopeshwa, ambapo ufuatiliaji wa vikundi vilivyopata mkopo unaendelea ili kuhakikisha kuwa fedha zinarejeshwa kwa wakati ili vikundi vingine viweze kukopeshwa.

Aidha, amesema serikali kwa kutambua kuwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu hawapati mikopo kwenye benki na taasisi nyingine za kifedha kwa kukosa dhamana za mikopo kwa sababu ya kuwa na mitaji midogo isiyowawezesha kupata mikopo kwenye taasisi hizo ndipo Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake, Vijana na watu wenye Ulemavu ilianzishwa kwa lengo la kuwainua kiuchumi kwa madhumuni ya kupambana na umaskini na kutatua changamoto wanazikabiliana nazo katika maisha yao ya kila siku.

“Mifuko hii huwanufaisha wananchi waliojiunga katika vikundi venye shughuli za ujasiriamali au vinavyokusudia kuanzisha shughuli za ujasiriamali mdogo au wa kati,”aliongeza Ngalisoni.

Hata hivyo, Mkuu wa wilaya hiyo, Mhandisi Zephania Chaula amesema, utoaji wa mikopo ungeongezeka kutoka sh.milioni tano mwaka 2013-2014 hadi kufikia zaidi ya sh.milioni 200 kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020.

Amesema, Serikali ya Awamu ya Tano inafanya kazi kwa vitendo zaidi kama inavyojieleza yenyewe, kwani ikisema inatenda na ikiahidi inatekeleza tena kwa wakati ili kuharakisha maendeleo ambayo wananchi waliyakosa kwa kipindi kirefu.