December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sillo:Kamati haitakuwa kikwazo kwa miradi

Judith Ferdinand, Timesmajira Online,Mwanza

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti haitakuwa kikwazo kwa miradi ya maji inayotekelezwa na mipya itakayoanzishwa na serikali huku ikieleza kuwa mradi wa maji Butimba utamaliza changamoto ya maji mkoani Mwanza.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Daniel Sillo wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kamati hiyo kutembelea na kukagua utekelezaji wa mradi wa chanzo kipya cha maji Butimba ambao mpaka sasa umefikia takribani asilimia 99 ya utekelezaji wake.

“Sisi kama kamati kazi yetu ni kutenga fedha katika miradi ya sekta zote ikiwemo miradi hiyo muhimu ya maji,hatutakiwa kikwazo kwa miradi mingine pengine inaendelea hata ile mipya ambayo itaibuliwa katika maeneo mbalimbali,”ameeleza Sillo.

Akizungumza mradi wa chanzo kipya cha maji Butimba Sillo ameeleza kuwa utakidhi mahitaji na kutatua changamoto ya maji iliokuwepo kwa wakazi wa Jiji la Mwanza na Wilaya jirani mkoani humo ambapo ambao umemtumia
takribani bilioni 82 huku kamati hiyo imeridhishwa na kazi ambayo inaendelea kufanywa katika mradi huo.

“Ni mradi ambao ukikamilika vizuri na kwa namna unavyoenda na umeisha fika hatua nzuri utakidhi mahitaji ya wananchi wa Mwanza kama ambavyo tumesikia kuna matenki kule Nyegezi na Igoma,maji haya yatatatua changamoto ya maji safi na salama,”.

Kwa upande wake Waziri wa Maji Juma Aweso ameeleza kuwa Jiji la Mwanza lilikuwa na changamoto ya maji kwa sababu mahitaji yake ni lita milioni 172 huku chanzo cha maji Capripoint kina uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 90 kwa siku hivyo kulikuwa na upungufu wa maji ambayo waliokuwa wakipata watu siyotoshelevu.

“Maelekezo ninayoyatoa kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA),mradi umekamilika isitokee sababu isiyo kuwa na ulazima watu kutounganishiwa maji,mtu anataka kuunganishwa maji aunganishiwe kwa muda mfupi ili watu wa Jiji la Mwanza waweze kupata maji safi na salama na yakutosheleza,”ameeleza Aweso.

Ameeleza kuwa muelekeo wa Wizara ya Maji ni ujenzi wa miradi ya maji ya kimkakati sasa hivi wana miradi ya Miji 28 katika maeneo ambayo wameainisha yalikuwa na changamoto kubwa ya maji.

“Kila eneo sasa lina Mkandarasi katika miradi hii ya Miji 28 na tunatumia chanzo toshelevu kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto ya maji,tumepewa maelekezo na Rais ifikapo 2025 asilimia 85 ya upatikanaji wa maji vijijini na asilimia 95 ya upatikanaji wa maji Mjini,”ameeleza Aweso.

Kwa sasa Wana asilimia 88 ya upatikanaji wa maji Mjini na asilimia 77 ya upatikanaji wa maji vijijini na wana miradi zaidi ya 244 ambayo wanatekeleza.

“Kukamilika kwa miradi hii 244 mjini tutafikia hii asilimia 95 ya upatikanaji wa maji Mjini lakini tuna miradi ambayo tunatekeleza vijijini zaidi ya 1500 na mkakati ni kuhakikisha miradi hii tunaisimamia na kukamilika kwa wakati ili kufikisha asilimia 85,”ameeleza Aweso.

Pia ameeleza kuwa wanavijiji takribani 2000 ambavyo vinapata maji ambayo siyo ya uhakika hivyo maelekezo wanayoyatoa kuwa Rais amewapatia magari ya kuchimba visima kila Mkoa hatutegemei wahandisi wa mikoa ama Wilaya ambapo magari yapo wawe wameyapaki lazima yatumike kwa ajili ya uchimbaji wa visima na watu waweze kupata huduma ya maji safi na salama.

Meneja Miradi wa MWAUWASA Celestine Mahubi ameeleza kuwa katika mradi huo una hatua kama nne kwa ajili ya kuchukua maji ziwani na baada ya kuyachukua wanayapeleka kwenye mtambo,kisha kwenye matenki na baada ya hapo yanaenda kwa wananchi.

“Vitu vyote vimeisha fanyika na vinaendelea kufanya kazi ambapo kwenye chanzo cha maji bomba limelazwa kilomita moja kutoka nchi kavu mpaka majini,”ameeleza Celestine.

Mradi huo gharama yake ni Euro milioni 31 ambapo kwa thamani ya kipindi wakati mradi unaanza kwa fedha za kitanzania ni sawa na bilioni 69 lakini kwa thamani ya kipindi hiki ni sawa bilioni 82 kwa sababu thamani imeongezeka.