December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge wa Jimbo la Momba, David Silinde (CHADEMA)

BREAKING NEWS: Silinde ahama Chadema, aomba kujiunga CCM

Na Doreen Aloyce, Timesmajira Online, Dodoma

MBUNGE wa Jimbo la Momba, David Silinde ametangaza rasmi kuhama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kuomba kujiunga Chama cha Mapinduzi (CCM).

Silinde amesema kuwa, uamuzi huo ni baada ya kutafakari kwa miezi miwili na kujiridhisha na utendaji kazi wa Rais wa Awamu ya Tano, Dkt. John Magufuli uliotukuka hivyo kuamua kumuunga mkono juhudi zake.

Uamuzi huo wa kujiunga na CCM, ameutangaza jioni ya leo Bungeni Dodoma wakati alipokuwa akichangia azimio la kumpongeza Rais kwa kupambana na janga la Corona hapa nchini.

Amesema, kwa uongozi wa Rais alipaswa kuongoza hata miaka ishirini mbele maana amekuwa akijibu hoja kwa vitendo jambo ambalo wapinzani wengi wamemuunga mkono kwani yale waliyoyahitaji ndiyo anayoyatekeleza.

“Hatuko tayari kuona upinzani unabomoa nchi, mfano kwenye hili janga la Corona Rais Magufuli amekuwa hodari na kusimamia maslahi ya taifa, nimeridhishwa sana na uimara wa Chama cha Mapinduzi “amesema Silinde na kuongeza.

“Nitaenda kuwaeleza Watanzania ukweli wote kuhusu Chadema nawajua ndani na nje mambo ambayo wamekuwa wakiwatendea wananchi na nitazidi kuelezea uzuri wa Rais wetu kwani amefanya kazi kwa vitendo na nampongeza sana “

Silinde amekiomba chama hicho kumpokea na kumpa ushirikiano kwani yupo tayari kukitumikia kwa moyo mkunjufu ili kumsaidia Rais kutekeleza majukumu yake.