January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Siku ya lishe ya Kijiji yaadhimishwa

Na Israel Mwaisaka, TimesMajira Online, Nkasi

KIJIJI cha Nkomolo wilayani Nkasi jana kimeadhimisha siku ya afya na lishe kwa kutoa elimu kwa vitendo namna ya kuandaa vyakula vilivyokamilika katika mlo kamili ili kuweza kupambana na tatizo la udumavu hasa kwa Watoto.

Maadhimisho hayo yamefanyika katika kituo cha afya Nkomolo ambapo Wazazi wa kike na wa Kiume wameweza kupata elimu ya kutosha na wengi kuahidi kwenda kuifanyia kazi elimu hiyo ili kukabiliana na tatizo hilo la udumavu.

Afisa mtendaji wa kijiji hicho Jenimery Julius Kalelwa amesema kuwa wao kama kijiji wamejipanga kutekeleza mpango wa lishe bora katika kijiji hicho na kuwa elimu wanayoitoa inakwenda kwa vitendo lakini pia wanaandaa vyakula ambavyo vinaliwa pamoja kwenye hafla hiyo ikiwa ni pamoja na wale wanaokuwepo clinic kwa siku hiyo ili kuweza kuupata uhalisia wa vyakula hivyo vilivyoandaliwa kitaalamu.

Amesema kuwa jamii yao inazungukwa na vyakula vingi kwa maana ni wazalishaji wakubwa wa nafaka na ufugaji wa mifugo mbalimbali lakini kinachokosekana miongoni mwao ni elimu sahihi ya matumizi ya vyakula hivyo kinachopelekea wao kupata udumavu.

Afisa mtendaji wa kata ya Nkomolo Agatha Lupepo kwa upande wake amesema kuwa kata yake imeanza kuutekeleza mpango huo wa lishe kwa vitendo na kuwa zoezi hilo litafanyika katika vijiji vyote vilivyopo katika kata ya Nkomolo.

Amesema kuwa mkoa Rukwa hususani wilaya Nkasi inazalisha chakula kingi na cha kutosha lakini udumavu upon a kuwa tatizo lipo kwenye matumizi sahihi ya vyakula hivyo na kuwa kama elimu hiyo itaendelea itasaidia kuweza kuondoa kabisa tatizo la udumavu kwa wakazi wa kata ya Nkomolo.

Awali Mwenyekiti wa kijiji hicho Spesioza Kauzeni alidai kuwa wao wameamua kuitenga siku hiyo ya afya na lishe ili kuweza kukabiliana na tatizo la udumavu na kuwa hakuna sababu ya kuwepo kwa watu wenye udumavu wakati vyakula vipo.

Amedai kuwa wataendelea kutoa elimu hiyo mara kwa mara hasa kwa kina Mama wanaoenda Clinic kwa shughuli mbalimbali za uzazi kuhakikisha elimu sahihi ya matumizi ya vyakula katika kukabiliana na tatizo hilo l

Baadhi wa Wananchi waliohudhiria siku hiyo ya afya na lishe wamedai kuwa watakwenda kuitumia elimu hiyo vizuri ili kuweza kuondokana na tatizo hilo la udumavu ambalo kimsingi wamesema linaweza kuepukika

Mkoa Rukwa ni moja ya mikoa inayotajwa kuwa na tatizo kubwa la udumavu licha ya mkoa huo kuwa na uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula