Na Hadija Bagasha, Timesmajiraonline,Tanga
WANANCHI mkoani Tanga, wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanya ziara yenye mafanikio makubwa mkoani humo, ambayo itachochea kukua kwa uchumi wa mkoa hu pamoja na mtu mmoja mmoja.
Wananchi hao walitoa pongezi hizo hivi karibuni wakati wakizungumza na majira kwa nyakati tofauti kuhusiana na ziara ya siku saba ya Rais Samia mkoani humo.
Katika ziara hiyo Rais Samia alizindua miradi mbalimbali ya maendeleo na kuzungumza na wananchi. Aidha kupitia ziara hiyo, Rais Samia alijionea jinsi fedha za Serikali ambazo zimekuwa zikipelekwa na Serikali mkoani humo zinavyotekeleza yale yaliyokusudia.
“Imekuwa ziara ya mafanikio makubwa kwa mkoa wa Tanga, kitendo cha Rais kukaa mkoani kwetu kwa siku saba inaonesha jinsi alivyokusudia kuleta maendeleo kwa mkoa wetu,” alisema Mussa Abdallah na kuongeza;
“Ameweza kutembelea wilaya zote na kila wilaya amezindua miradi mikubwa. Hili ni jambo la kujivunia, kwani tuliyoyashuhudia kwa kipindi chake cha miaka minne ya uongozi wake ni makubwa.”
Juzi, Rais Samia amehitimisha ziara yake ambapo alizindua na kukagua miradi mbalimbali yenye thamani ya takribani sh. trilioni 3.1 fedha ambazo zimeelekezwa Mkoani Tanga kwa ajili ya maendeleo katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake.
Katika ziara yake Rais Dkt. Samia alifanya ukaguzi wa maboresho ya gati mbili mpya katika bandari ya Tanga.
Alisema uwekezaji katika bandari za nchi ni njia ya kukuza uchumi, kuongeza ajira, na kuboresha biashara ya kimataifa.
Akizungumza kuhusu maendeleo ya sekta ya bandari, Rais ameeleza kuwa Serikali inaendelea na juhudi za kuboresha miundombinu ya bandari ili kuongeza ufanisi na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Alieleza kuwa uwekezaji huo utasaidia kuongeza mapato ya taifa kupitia biashara na usafirishaji wa bidhaa.
Aidha, Rais alisisitiza kuwa Serikali inahakikisha kuwa uwekezaji katika bandari unazingatia maslahi ya taifa kwa kuhakikisha kuwa mikataba ya uwekezaji inakuwa yenye manufaa kwa Watanzania wote.
Alibainisha kuwa ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali ni muhimu katika kuleta maendeleo endelevu katika sekta ya uchukuzi na usafirishaji.
Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya upanuzi wa bandari, ikiwemo Bandari ya Dar es Salaam, Tanga, na Mtwara, ili kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha biashara kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
. Rais ameahidi kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji huku ikihakikisha kuwa Watanzania wananufaika na maendeleo haya kupitia ajira, biashara, na huduma zinazotokana na uwekezaji wa bandari.
More Stories
DAWASA:Upatikanaji huduma ya maji Dar asilimia 93
Mmoja afariki,33 wajeruhiwa ajali ya tingatinga na coaster
Tume ya Madini yafungu kamfanikio uongozi wa Samia