Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya
HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbeya imepokea zaidi ya shilingi bilioni 43 kutoka Serikali Kuu na wadau wa maendeleo katika siku 100 za uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita kipindi cha pili, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na shughuli za kawaida za halmashauri hiyo.
Imeelezwa kuwa fedha hizo, zilizopokelewa kuanzia Oktoba 2025 hadi Februari 2026, zimeiwezesha halmashauri hiyo kupata mafanikio makubwa katika uboreshaji wa huduma za kijamii na kiuchumi kwa wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari Januari 29, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Bi. Erica Yegella, amesema mafanikio hayo ni matokeo ya siku 100 za kwanza za uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kipindi chake cha pili kufuatia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Yegella amesema kati ya fedha hizo, zaidi ya shilingi bilioni 38 zimetolewa na Serikali Kuu, shilingi milioni 700 zimetoka kwa wadau wa maendeleo, huku shilingi bilioni nne zikitokana na mapato ya ndani ya halmashauri.
Amesema fedha hizo zimetumika kulipa mishahara ya watumishi wa umma, kuimarisha elimu bila malipo, kuboresha huduma za afya, kutekeleza miradi ya maendeleo ngazi ya jamii pamoja na kuimarisha utawala na huduma za elimu.
“Kiasi hiki cha fedha kimeleta tija kubwa katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia huduma muhimu za kijamii na kiuchumi,” amesema Yegella.
Kuhusu sekta ya elimu na afya, Yegella alisema halmashauri imefanikiwa kujenga vyumba 12 vya madarasa, matundu 18 ya vyoo katika shule tano za msingi, kujenga shule mpya ya awali, kukarabati shule moja ya msingi, pamoja na kukamilisha vituo vya afya vya Ulenje na ujenzi wa kituo cha afya cha kimkakati cha Isuto.
Aidha, amesema zahanati tisa zimekamilishwa na vifaa tiba vimenunuliwa kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya pamoja na zahanati mpya zilizofunguliwa katika kipindi cha siku 100.
Katika sekta ya afya, Yegella amesema
zaidi ya shilingi bilioni moja zimetolewa na Serikali Kuu, wahisani na kupitia mapato ya ndani, ambapo shilingi milioni 250 zimetumika katika ujenzi wa kituo cha afya cha kimkakati cha Isuto.
Ameongeza kuwa vituo vitatu vya afya vimekamilishwa, ikiwemo Ulenje (shilingi milioni 600), Mbalizi (shilingi milioni 50) na Swaya (shilingi milioni 15), huku utekelezaji wa miradi mingine ukiendelea.
Pia ameongeza zaidi ya shilingi milioni 580 zimetumika kukamilisha zahanati tisa katika vijiji vya Hashungu, Nsongwi Juu, Jojo, Masewe, Mwashoma, Ifiga, Isangala, Iyunga Mapinduzi na Itambalila, pamoja na shilingi milioni 200 zilizotumika kununua vifaa tiba kwa Hospitali ya Wilaya na vituo vipya vya afya vinavyotarajiwa kufunguliwa hivi karibuni.

Yegella amesema katika kipindi hicho halmashauri imefanikiwa kufungua zahanati mpya sita za Itete, Jojo, Masewe, Iyunga Mapinduzi, Mapogoro na Madugu, huku zahanati saba nyingine zikitarajiwa kufunguliwa.
Mwisho, amewashukuru wadau wa maendeleo kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuchochea maendeleo, akisema mapato ya ndani ya halmashauri yameendelea kusaidia utekelezaji wa elimu bila malipo, ukamilishaji wa miradi ya afya na elimu pamoja na ulipaji wa mishahara ya watumishi.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina