March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Siku 100 za Rais Samia zaleta neema Igunga

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Igunga

SIKU 100 baada ya kuingia madarakani kwa awamu ya pili, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan,neema imewapata wakazi wa Mji wa Igunga mkoani hapa kwa kuwawezesha kupata huduma ya maji kwa saa 24 kila siku.

Akizungumza Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Igunga (IGUWASA) Alex Ntonge,amebainisha kuwa maboresho makubwa ya miundombinu na kupanuliwa kwa mradi wa maji ya Ziwa Victoria kumewezesha wakazi wote wa mji huo na maeneo jirani kupata huduma ya maji safi na salama wakati wote, kwa saa 24 kila siku.

‘Katika siku 100 za kwanza za Rais,zimeleta neema, mabilioni aliyotuletea yameendelea kuboresha huduma ya maji na usafi wa mazingira wa mji wote,”amesema.

Amesema,zaidi ya asilimia 98 ya wakazi wote wa Mji huo ikiwemo Kata za Mbutu, Mwamashimba, Isakamaliwa na Mwalala, wamenufaika na maboresho makubwa ya huduma hiyo yaliyofanywa na IGUWASA.

Pia amesema,mahitaji ya maji katika Mji huo ni lita za ujazo 6,700 kwa siku lakini kutokana na maboresho yaliyofanywa, sasa mamlaka inazalisha lita za ujazo 8,500 kwa siku, hivyo kuwa na maji ya ziada.

Aidha amesema, jitihada za kusogeza huduma ya maji safi na salama kwa wananchi na katika maeneo yote ambayo hayajafikiwa na mtandao huo zimeendelea kufanywa na IGUWASA kupitia fedha za ndani na miradi mingine inayofadhiliwa na Serikali.

Kwa upande wa usafi wa mazingira amesema serikali imewezesha magari 2 maalumu kwa ajili ya uondoshaji majitaka katika makazi ya wananchi kwa njia iliyo bora, salama na endelevu na kazi inaendelea.

Hata hivyo amesema serikali iliwapatia kiasi cha shilingi bilioni 1.86 kwa ajili ya kufanikisha mradi wa uboreshaji huduma ya usafi wa mazingira na kutibu maji taka na shilingi bilioni 3.47 za mradi wa uboreshaji mfumo wa uzalishaji maji.

Ntonge amefafanua kuwa mradi wa ukarabati wa mfumo wa uzalishaji maji ulilenga kuboresha bwawa la Bulenya na mfumo wa kutibu maji wa Igogo na ujenzi wa mtandao wa uhakika wa kusafirisha maji hayo.