Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
ILI kukabiliana na changamoto ya uwepo wa wanafunzi wanaohitimu Elimu ya msingi wakiwa hawajui kusoma Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndani ya siku 100 imetekeleza mpango mkakati wa kisayansi wa kujenga umahiri wa kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) kwa Watoto wa Elimu ya awali na darasa la kwanza hadi la pili.
Hayo yamesemwa jijini hapa leo tarehe 31Januari, 2026 na Waziri wa Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa ahadi na Rais Samia ndani ya siku 100 za uongozi wake katika kipindi cha pili.
Prof.Mkenda amesema kuwa Mpango mkakati huo unaotekelezwa ndani ya miaka mitano unalenga kuhakikisha kila mtoto anamudu stadi za Msingi afikapo darasa la tatu kupitia njia za kisayansi shirikishi na bunifu.

“Mtoto anaanza Darasa la Kwanza akiwa na umri wa miaka sita, Darasa la Pili miaka saba, na Darasa la Tatu miaka minane, ni dhahiri kuwa mkakati huu umejikita zaidi katika elimu ya awali, Darasa la Kwanza na Darasa la Pili, ili afikapo Darasa la Tatu mtoto awe tayari amepata mafanikio makubwa katika kusoma, kuandika na kuhesabu,”amesema.
Aidha Prof.Mkenda amewataka wakuu wa shule kuzingatia kikamilifu kalenda ya masomo na ufundishaji inayotolewa na Kamishna wa Elimu, ili kuwapatia wanafunzi muda wa kupumzika, hususan katika vipindi vya likizo.
“Hatua hii inalenga kulinda haki za wanafunzi, kuboresha mazingira ya ufundishaji na kujenga mfumo wa elimu unaozingatia ustawi wa mtoto na ubora wa elimu kwa ujumla,”amesema
Vilevile Prof.Mkenda amesema kuwa katika kipindi cha siku 100 za Rais Samia Serikali kupitia Wizara hiyo imenunua na kusambaza vifaa vya kidijiti na saidizi vyenye thamani ya shilingi bilioni 5.4 kwa walimu wa shule za msingi na sekondari, wakufunzi pamoja na walimu tarajali wenye ulemavu katika vyuo vya ualimu nchini, kwa lengo la kurahisisha ujifunzaji na ufundishaji jumuishi.
Prof. Mkenda amesema jumla ya wanufaika 1,055 kutoka Halmashauri 104 nchini wamenufaika na mpango huo, ambapo vifaa vilivyosambazwa ni pamoja na kompyuta mpakato 680, vifaa tisa vya Brain Note Touch Pass, vinasa sauti (voice recorders) 377, tablet 196 kwa wanaotumia lugha ya alama, mashine 30 za Perkins Braille, vifaa 101 vya kusaidia kusikia pamoja na mashine za Everest Drill Embosser.
Ameeleza kuwa mashine hizo zinawezesha walimu wasioona kuchapa maandishi kwa kutumia nukta nundu (Braille) na baadaye kuchapisha maandishi ya kawaida yanayoweza kusomwa na wanafunzi wengine, hivyo kuimarisha ushiriki sawa katika ufundishaji.
Aidha, amesema kuwa Serikali imekuwa ikitoa vifaa saidizi na vitabu maalum kila mwaka kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita, huku Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) ikihakikisha vitabu vinachapishwa kwa maandishi makubwa kwa wenye uoni hafifu na kwa nukta nundu kwa wasioona kabisa.


More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina