December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

SIDIFA watakiwa kuwekeza kwenye soka la Wanawake

Na Jumbe Ismailly, Singida

CHAMA Cha Mpira wa miguu katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida (SIDIFA) kimeshauriwa kuangalia uwezekano wa kuwekeza nguvu nyingi kwenye mchezo wa mpira wa miguu kwa wanawake.

Wito huo umetolewa na Kaimu Afisa vijana Mkoa wa Singida, Fedrick Ndahani alipokuwa akikabidhi zawadi mbalimbali kwa washindi wa shindano ya Bonanza la kupiga vita vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia lililofanyika katika uwanja wa michezo wa kumbukumbu ya Liti mjini hapa.

Amesema, uzoefu unaonesha kuwa kwa muda mrefu sasa wanawake wamekuwa hawashirikishwi katika michezo hivyo ni wakati muafaka kutumia fursa ya rais wa Awamu ya sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kuwashirikisha katika michezo mbalimbali.

“Nitoe wito kwa SIDIFA, Mkurugenzi na Afisa Michezo kwamba kwa sasa tunaye rais wa Tanzania ambaye ni mwanamke, hivyo kama rais wa Tanzania ni mwanamke, basi tuweke nguvu sana kwenye michezo hususani ya wanawake,”.

Kutokana na kuwasahau na kuwaweka nyuma wanawake katika suala la michezo hivyo iwe ni chachu kubwa kuhakikisha kwamba wanawake wanashiriki vizuri kwenye michezo ili waweze kutumia fursa hiyo ya rais kuwa mwanamke.

Hata hivyo Ndahani ametumia fursa hiyo pia kutoa wito kwa Mashirika na taasisi za nje na ndani ya nchi kwamba isiwe mwisho kuunga mkono jitihada za serikali katika kuendeleza sekta ya michezo ili kuhakikisha kwamba michezo pamoja na matamasha ya aina hiyo yakiendelea kufanyika kwenye maeneo ya Manispaa ya Singida na Mkoa mzima wa Singida.





Baadhi ya vijana walioshiriki shindano la kula Tikitimaji kwenye bonanza la kupiga vita unyanyasaji wa kijinsia lililofanyika katika uwanja wa kumbukumbu ya michezo ya Liti, mjini Singida.
(Picha n Jumbe Ismailly).

“Lakini nitoe wito pia kwa mashirika na taasisi za nje na ndani ya nchi kwamba isiwe mwisho kuunga mkono jitihada za serikali katika kuendeleza sekta ya michezo ili kuhakikisha michezo pamoja na matamasha yakiendelea kufanyika katika Manispaa ya Singida na Mkoa mzima ili lengo letu la kutokomeza ukatili wa kijinsia liweze kufikiwa,” amesema kiongozi huyo.

Akitoa taarifa ya michezo ya Bonanza hilo lenye lengo la kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia, Mkuruenzi wa Fedha wa Asasi ya Umoja wa Mataifa –YUNA –Tanzania, Ally Mwamzola amesema, lengo kuu la bonanza hilo lilikuwa ni namna gani wanaweza kuwashirikisha vijana na wanaume katika kupinga ukatili wa kijinsia unaotokea kwenye maeneo tofauti.

Mwamzola ambaye pia ni Mwakilishi katika Mtandao wa Men Engage amebainisha kuwa, kuna baadhi ya wanaume ambao hufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na wenza wao lakini wamekuwa wakishindwa kupata nafasi ya kwenda kuyasemea kwenye mamlaka zinazohusika kupinga unyanyasaji huo.

Aidha amesisitiza wanawake pamoja na watoto wamekuwa wakifanyiwa vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia lakini wanashindwa kupata fursa ya mahali pa kuyapeleka na kuyaweka wazi.

Bonanza hilo la kupinga ukatili wa kijinsia limeshirikisha michezo mbali mbali ukiwemo mpira wa miguu, kuvuta kamba, kunywa soda, kula tikiti maji bila kulishikilia, kufukuza kuku na kula mkate mkavu bila chai.