November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Shule zote za msingi Ilala kupata madawati

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar

HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam, imejipanga kupunguza changamoto ya ukosefu wa madawati pamoja na viti kwa shule zote za msingi zilizopo Wilaya ya Ilala hivi karibuni.

Hayo yamesemwa Desemba 20,2023 na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, wakati akikabidhi viti na meza 17,500 vitakavyoenda kutumika kwa shule za sekondari za Kata zilipo Halmashauri Jiji la Dar es Salaam hafla iliofanyika shule ya sekondari Pugu iliyopo jijini humo.

Ameeleza kuwa wameona shule zao za msingi zilizopo katika Wilaya ya Ilala zikiwa na upungufu wa madawati 20,000,hivyo watapeleka madawati katika shule zote za msingi zilizopo kwenye Wilaya hiyo.

“Tayari mchakato wa utengenezaji umeshaanza na unaendelea,baada ya kukamilika madawati hayo yatawafikia watoto wetu ili wawe na mazingira mazuri ya kusoma na hili ni agizo la Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Tamisemi la kutumia zaidi ya asilimia 70 ya pato tunalopata,”amesema Mpogolo.

Pia amewatoa hofu walimu wa shule za msingi wilayani humo kwa kuwaeleza kuwa serikali inaenda kuwaboreshea mazingira ya ufanyaji kazi ikiwa ni pamoja na upelekaji wa viti na meza katika shule zenye upungufu wa samani hizo pamoja na uboreshaji wa ofisi za walimu.

” Baada ya kumaliza hili la watoto wetu kuwawekea mazingira mazuri ya kusoma,tunaenda kuhakikisha walimu wanapata viti na meza kwa Halmashauri nzima kwani wanafanya kazi kubwa sana halafu unakuta kuna sehemu walimu wanakaa wawili katika kiti kimoja hatupo tayari kuliona hilo kama Jiji,”amesema Mpogolo.

Sanjari na hayo ameeleza kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, imeendelea kufanya vizuri katika ukusanyaji wake wa mapato, ambapo hivi sasa ina uwezo wa kukusanya hadi bilioni 8 kwa mwezi, ikiwa tofauti na awali ilikuwa ikikusanya kiasi cha bilioni 4 hadi 5 na kudai kuwa kiasi hicho kilikuwa hakistahili kwa halmashauri hiyo.

Ambapo amesema, ili Halmashauri iliweze kufanya maendeleo kwa watu wake ni lazima iwe na uwezo wa ukusanyaji mzuri wa fedha.

Hivyo amempongeza, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Jomaary Satura na Wabunge wote wa Wilaya ya Ilala, kwa ushirikiano ambao wameendelea kutoa katika Wilaya hiyo, hali inayochochea ukuaji wa maendeleo kwa kasi kubwa.

Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mbunge wa Jimbo la Ukonga Jerry Silaa amempongeza Mkuu huyo wa Wilaya kwa kazi nzuri ambayo ameendelea kufanya ya kuhakikisha analeta maendeleo kwa wananchi wake.

Naye Diwani wa Kata ya Pugu Imelda Samjela amemshukuru Rais kwa kumteua Mkuu wa Wilaya ya Ilala na Mkurugenzi wa jiji la hilo kwani wamekuwa mstari wa mbele kuleta maendeleo katika Wilaya hiyo kwani Ilani ya uchaguzi ya CCM imetekelezeka kwa asilimia kubwa na matokeo yameonekana kupitia viongozi hao.

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, hivi sasa inao uwezo wa kutengeneza viti na meza kwa Sh.80,000, tofauti na awali vilikuwa vikitengenezwa kwa Sh. 135,000, ambapo imeweza kuokoa kiasi cha milioni il 800.