November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Thobias Mwilapwa akikabidhi Mwenge wa Uhuru kwa Kaimu Mkuu wa wilaya ya Pangani, Toba Nguvilla.

Shirikianeni na polisi kuwaibua wauza madawa ya kulevya-Luteni Mwambashi

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online-Pangani

WANANCHI wametakiwa kushirikiana na Jeshi la Polisi nchini kuwaibua watu wanaojihusisha na uuzaji wa dawa za kulevya ikiwemo bangi, mirungi na heroine ili kuokoa nguvu kazi ya vijana ambao wamekuwa wakitumbukia kwenye matumizi ya dawa hizo.

Hayo yalisemwa na kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2021, Josephine Paul Mwambashi wakati alipofika wilayani Pangani mkoani Tanga.

Kiongozi huyo amesema, jamii inapaswa kuona ipo haja ya kufichua na kutoa taarifa kutoka kwenye maeneo yao pindi wanapobaini kuwa na mtu anayejihusisha na uuzaji wa dawa hizo.

“Wananchi tunapaswa kuwaibua watu wanaojihusisha na uuzaji wa madawa ya kulevya yamekuwa yakitupotezea nguvu kazi ya Taifa letu tunapaswa kulipiga vita wakati wote, “alisisitiza Mwambashi.

Kiongozi Mwanbashi alisema, mbio hizo za Mwenge wa Uhuru zimekuwa zikitumika kuelimisha wananchi katika maeneo yote nchini jinsi ya kupambana na maradhi yanayotishia ustawi wa watu kama vile UKIMWI, Malaria na kuhamasisha wananchi kushiriki vita dhidhi ya rushwa na matumizi ya dawa za kulevya.

Hata hivyo, Mwenge wa Uhuru ukiwa wilayani Pangani umekagua, umezindua na kuweka jiwe la msingi katika miradi 7 yenye thamani ya bilioni 1.5 ikiwemo ya maji, barabara, uzinduzi wa miradi mbalinbali ikiwemo ya vijana.

Aliongeza kuwa, Mwenge wa Uhuru na mbio zake zimekuwa na faida kwa taifa ikiwemo kuendelea kuhamasisha wananchi kushirikiana na Serikali yao katika kubuni na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mbio za Mwenge wa Uhuru zitaendelea kuwakumbusha na kuwahamasisha wananchi na viongozi kote nchini, kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI, ugonjwa Malaria, mapambano dhidi ya matumizi ya Dawa za Kulevya, Mapambano dhidi ya Rushwa na kuhamasisha Wananchi juu ya Lishe bora kwa afya imara.