Na Omary Mtamike,TimesMajira Online, Mbeya
TAASISI ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Utafiti la (CIAT) wamewasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi wa utafiti wa malisho yaliyoboreshwa uliotekelezwa kwa miaka 4 katika kanda ya nyanda za juu kusini.
Mgeni rasmi katika kikao cha kuwasilisha taarifa hiyo kilichofanyika kwenye Ukumbi wa kituo cha Mafunzo cha wakulima kilichopo Tukuyu jijini Mbeya ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Dkt. Vincent Anney amezipongeza pande zote kwa hatua hiyo ambapo ametoa rai kwa watekelezaji wa matokeo ya utafiti huo kuhakikisha elimu na ujuzi uliopo kwenye taarifa hiyo unaenea kwa wafugaji wote nchini.
“Ili tuwe na ufugaji wenye tija ni lazima utafiti unaombatana na majaribio ufanyike kama ambavyo mradi huu umefanya kwa kushirikiana na Serikali hivyo nashauri iundwe kamati maalum ya kufuatilia uendelezaji wa yote yaliyofanyika wakati wa mradi ili tutumie fursa tuliyoipata kusonga mbele badala ya kusubiri mradi mwingine” Amesema Dkt. Anney.
Dkt. Anney amebainisha kuwa mradi huo umewahamasisha wafugaji kuzalisha malisho ambayo yameleta tija na kuongeza uzalishaji wa mazao yanayotokana na mifugo hivyo ametoa rai kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuweka mipango madhubuti ya kutafuta masoko ya mazao hayo.
“ Uzalishaji mkubwa wa malisho yaliyoboreshwa unaofanywa na wafugaji wetu hivi sasa kupitia mradi huu umesababisha uzalishaji wa maziwa mengi hivyo wafugaji wameanza kukosa soko la maziwa hayo na kwa sababu hawatumii nguvu kubwa kwenye kuyazalisha tofauti na ilivyokuwa awali wanaweza kuona hiyo hali ni ya kawaida kwa hiyo ni lazima tuwasaidie ili maziwa hayo yawaletee tija ya kutosha” amesisitiza Dkt. Anney.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) Prof. Erick Komba mbali na kuonesha furaha ya kuhitimisha mradi huo kwa mafanikio ameweka wazi kuwa Taasisi yake ipo tayari kushirikiana na wadau wote wenye lengo la kuendeleza sekta ya mifugo nchini kama ilivyofanya na Shirika hilo.
“Mbali na utafiti wa malisho, Taasisi yetu pia inafanya utafiti katika vyakula vya mifugo na ulishaje wake, Uzalishaji, uzazi, afya ya mifugo na haki za wanyama ambapo ili kutekeleza shughuli zake Taasisi yetu inapata fedha kutoka Serikalini, vyanzo vyetu vya ndani na kupitia wadau wa maendeleo kama CIAT na wengineo” Ameongeza Prof. Komba.
Prof. Komba amesema kuwa hivi sasa Taasisi yake inaendelea na tafiti mbalimbali ikiwa ni pamoja na utafiti mpya unaolenga kutengeneza teknolojia na mtandao wa ushauri katika ubora wa maziwa ambao unafanyika katika kanda ya Mashariki ya Taasisi hiyo iliyopo mkoani Tanga, utafiti wa vyakula vya mifugo vinavyojumuisha michanganyiko ya bei rahisi inayompa mnyama afya bora.
“Lakini pia tuna majaribio mengi sana huko vituoni yanayohusu uzalishaji mifugo, matunzo ya mifugo, unenepeshaji, uchambuzi na kutathmini mifugo na mawe lishe katika eneo la ulaji na ukuaji wa mbuzi zoezi linaloendelea kwenye kituo chetu cha Kongwa” Amesema Prof. Komba.
Naye Mwakilishi wa Shirika la CIAT, Dkt. An Notenbaert ameishukuru Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa ushirikiano waliouonesha wakati wote wa kutekeleza mradi huo ambao pia ulilenga kufanya utafiti wa malisho bora kwa mifugo na kuandaa taarifa ya utafiti itakayotumiwa na watekelezaji wa Sera katika kuinua sekta ya mifugo nchini.
“Pia nitoe shukrani zangu kwa Shirika la IFARD kwa kukubali kutoa fedha za kutekeleza mradi huu hivyo iwaombe wafugaji na wazalishaji wa malisho ya mifugo nchini pamoja na mradi huu kufikia kikomo, waendelee kusambaza mbegu za malisho haya yaliyoboreshwa katika maeneo mengine yaliyosalia hapa nchini ili kila mfugaji anufaike na malisho haya” Amesema Dkt. Notenbaert.
Kwa upande wa mmoja wa wafugaji walionufaika kutokana na mradi huo kutoka mkoani Njombe, Juliana Mlagala amesema kuwa malisho hayo yaliyoboreshwa yamewaongezea ari ya kuendelea kufuga baada ya kuonesha matokeo chanya kwenye mifugo yao.
“Tangu tuanze kutumia malisho haya yaliyoboreshwa tumekuwa na uhakika wa chakula bora cha mifugo yetu na tumeokoa muda mwingi sana ambao zamani tulikuwa tunaupoteza kwenda kutafuta malisho ya mifugo yetu hivyo ninaomba Serikali iendelee kutuletea miradi ya aina hii ili tuendelee kunufaika kutokana na shughuli hizi za ufugaji” Amesema Mlagala.
Mradi wa Utafiti wa kilimo cha malisho yaliyoboreshwa bila kuathiri mazingira umetekelezwa na Shirika la kimataifa la Utafiti la CIAT kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya Idara ya Mafunzo, Utafiti na Ugani kupitia taasisi yake ya TALIRI ambapo umetekelezwa kwa miaka 4 katika Halmashauri 3 ambazo ni Mufindi, Njombe na Rungwe.
More Stories
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi
Mbunge Ndingo:CCM imejidhatiti kuwaletea maendeleo wananchi
SACP Katabazi: Elimu ya usafirishaji wa kemikali bado ni muhimu kwa watanzania