January 2, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Shirika la CDF laanzisha mradi wa kuzuia ukatili

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Shirika la jukwaa la Utu wa mtoto (CDF) imekuja na mradi mpya wenye lengo la kuhamasisha jamii kuzuia vitendo vya ukatili wa kingono kwa watoto hasa watoto wa kike kutokana na kuongezeka kwa wimbi la watoto wanaofanyiwa ukatili wa kingono.

Utafiti uliofanywa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) 2022 ulibaini kuwa zaidi ya 80% ya watoto wanapitia ukatili wa kingono nchini Tanzania na wahusika wakuu wanaofanya ukatili huu ni ndugu wa karibu au wakazi wa eneo hilo, walimu, dereva wa pikipiki (bodaboda) n.k.

Pia takwimu za utafiti wa Hali ya Idadi ya Watu na Afya (2023) inaonyesha 12% ya wanawake wenye umri wa miaka 15-49 wamewahi kufanyiwa ukatili wa kingono na 7% waliathiriwa na ukatili wa kingono katika miezi 12 kabla ya utafiti. 

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo,Mkurugenzi Mtendaji 

Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Koshuma Mtengeti  alisema Mradi huo utatekelezwa katika Wilaya ya Mpwapwa na utakuwa wa miaka miwili (2) ambapo utatekelezwa katika kata mbili za Wilaya ya Mpwapwa ambazo ni Pwaga na Lupeta. 

“Lengo kuu la Mradi huu ni kupunguza kuenea kwa vitendo vya ukatili wa kingono kwa watoto hasa watoto wa kike kwa kuhamasisha jamii kuzuia ukatili huo. Kupitia Mradi, shirika la CDF litafanya kazi na watoto walioko ndani ya shule, waalimu na menejimenti ya shule, viongozi wa serikali, wamiliki wa nyumba za kupanga, wahudumu wa afya, wazazi pamoja na vikundi vya kina baba ambavyo CDF inafanya navyo kazi katika kata hizi mbili.”

Mkurugenzi huyo alisema ili kufikia malengo ya Mradi huo, watafanya shughuli mbalimbali zikiwemo kuwajengea uwezo watoto kwa kuwapa elimu ya afya ya uzazi na namna ya kuzuia ukatili wa kingono, kuwajengea uwezo wahudumu wa afya ili waweze kutoa huduma bora na rafiki za afya ya uzazi kwa vijana balehe, kuwajengea uwezo wazazi, wamiliki wa nyumba za kupanga zilizo karibu na maeneo ya shule na walimu juu ya kulinda na kuzuia ukatili wa kingono kwa watoto, kuibua changamoto mbalimbali za ukatili wa kingono kwenye jamii, na kuelimisha jamii juu ya madhara ya ukatili kwa watoto kwa kutumia midahalo, vipeperushi, mikutano ya hadhara na vyombo vya habari.

“Tutashirikiana na watumishi mbalimbali wa Serikali katika halmashauri ya Mpwapwa waliopo katika ofisi ya Ustawi wa Jamii, idara ya Maendeleo ya Jamii, idara ya elimu, ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya, Dawati la polisi la jinsia na watoto, Mahakama ya Wilaya, watendaji Kata na Vijiji kutoka kata za Lupeta na Pwaga pamoja na wadau wote wa ulinzi wa mtoto waliopo katika Wilaya ya Mpwapwa”

Mbali na hayo Mtengeti alisema walikumbana na changamoto mbalimbali wakati wa utekelezwaji wa mradi huo hivyo aliwasihi watanzania wote kuzungumza na kupaza sauti kwa pamoja ili waweze  kusonga mbele na kushinda vita dhidi ya ukatili wa kijinsia .

Changamoto hizo ni kama ifuatavyo: “Jamii kutokuwa na elimu ya kutosha kujua madhara ya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto na wanawake, Mfumo dume unaochochea ukatili dhidi ya wanawake na watoto kama tafiti zinavyoonyesha kuwa wanawake walio kwenye uhusiano na wanaume ambao tabia na imani zao zinabeba na kushinikiza ubabe wa kiume zinapelekea kukosekana kwa usawa wa kijinsia na kusababisha unyanyasaji mwingi wa kijinsia kwenye familia”

“Uhaba wa maafisa ustawi wa jamii, maafisa ustawi wa jamii wana wajibu mkubwa kumsaidia mtoto aliyepitia ukatili kama kutoa ushauri, uendeshaji wa mashauri ya watoto na majukumu mengineyo lakini kuna uhaba mkubwa wa wataalam hawa pamoja na changamoto nyinginezo nyingi, lakini pia Kuongezeka kwa vitendo vya ukatili wa kingono vinavyopelekea maambukizi ya UKIMWI na magonjwa mengine ya zinaa.”

Aliendelea kutaja changamoto hizo ikiwemo “Sheria kutokuwa na adhabu kali kwa washtakiwa wa makosa ya ukatili wa kingono kwa Watoto na 

Jamii kuendelea kutumia mila potofu/kandamizi zinazomsababisha mtoto wa kike kubaguliwa na kutokuwa na haki ya usawa kwenye jamii”

Mbali na changamoto hizo Mtengeti alisema yapo mafanikio waliyoyapata kutokana na utekelezaji wa miradi yao kwa kipindi cha miaka 7. 

“Wanawake vijana na watoto 220 (152KE,68ME) waliongezewa uelewa na ujuzi juu ya haki za watoto, ukatili wa kijinsia na madhara yake, afya ya uzazi, uongozi, utoaji wa taarifa za ukatili na stadi za maisha zinazowawezesha kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili kama vile mimba za utotoni, ndoa za utotoni na magonjwa ya zinaa ikiwa ni pamoja na maambukizi ya VVU/UKIMWI, Wasichana 45 walioko nje ya shule kutoka kata za Kibakwe, Berege na Pwaga walipata mafunzo ya ujasiriamali, utafutaji masoko, na usimamizi wa biashara, 

wasichana 18 walipewa mafunzo ya ushonaji na kupewa mashine za kushonea (vyerehani) kwa ajili ya kupata kipato kitakachowasaidia kuendeleza maisha yao na watoto wao, Kati ya wasichana 45, wasichana 10 kutoka kata za Pwaga na Kibakwe waliunganishwa na taasisi ya fedha (CRDB-Mpwapwa) na kuongeza uelewa juu ya huduma mbalimbali za kifedha zinazolenga wanawake vijana kupata mikopo yenye riba nafuu zitakazowasaidia kujikwamua kiuchumi na kukuza biashara zao n.k”