Na Suleiman Abeid, Timesmajira Online Shinyanga
UONGOZI wa Serikali mkoani Shinyanga umeshauriwa kuandaa kongamano kubwa la michezo mkoani humo litakalowashirikisha wadau mbalimbali wa michezo ili kuweka mikakati ya jinsi ya kufufua mchezo wa mpira wa miguu na kuuwezesha mkoa huo kuwa na timu inayocheza Ligi Kuu ya NBC.
Ushauuri huo umetolewa na mmoja wa wadau wa michezo mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja kwenye maadhimisho ya “Simba Day” ambayo yamefanyika kwenye vijiji vya Kiinza na Nyanhembe katika kata ya Kilago Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga.
Mgeja amesema kwa takribani miaka minne sasa imepita bila mkoa wa Shinyanga kuwa na timu yoyote ya mpira inayocheza Ligi Kuu ya NBC hali ambayo imechangia kushusha ari na shamramshara za michezo katika mkoa huo.
“Naomba nichukue fursa hii kupitia sherehe hizi za “Simba Day” ambazo wapenzi wa timu ya Simba tunaadhimisha hapa leo kuwaomba viongozi wetu wa Serikali kuanzia ngazi ya wilaya na Mkoa wakae chini waweke mpango wa kuandaa kongamano kubwa la wadau wa michezo mkoani petu”
“Kongamano hili likiandaliwa sisi wadau wa michezo hususani wale wa mpira wa miguu tujadili jinsi gani tutaweka mikakati madhubuti ya kuzisaidia timu zetu zilizopo daraja la kwanza na Championship ili ziweze kupanda na kuingia Ligi Kuu ya NMB, hii itatusaidia kukuza vipaji vya michezo kwenye mkoa wetu” ameeleza Mgeja.
Amesema mkoa wa Shinyanga mbali ya kuwa na utajiri wa watu lakini pia una wafanyabiashara wakubwa na makampuni makubwa ya migodi ya madini ambayo yanaweza kuhamasishwa na kuchangia shughuli za michezo kwa kuzidhamini timu zilipo mkoani humo kuweza kufanya vizuri kwenye maashindano zinazoshiriki.
Kwa upande mwingine Mgeja ambaye pia ni mwenyekiti wa Taasisi ya Mzalendo Foundation yenye makazi yake wilayani Kahama amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyosimama kidete kuweka hamasa katika michezo hapa nchini ambapo amewaomba wadau wengine kuiga mfano huo wa Rais.
Katika shamrashamra hizo za “Simba Day” amewashauri mashabiki wa timu za Simba na Yanga kuendeleza utamaduni wa utani wa jadi badala ya kuzalisha na kukuza uadui kitu ambacho kitaurudisha mpira wa Tanzania katika ngazi ya chini na kushindwa kufanya vizuri kimataifa na kuitangaza Tanzania.
Mgeja ameviomba vilabu na wadau vya michezo nchini kuwekeza katika soka la wanawake na vijana ili kuweza kupata mafanikio makubwa na mazuri kama yalivyo mataifa ya Senegal, Africa Kusini, Tunisia na mengine ambayo yamejikita katika vituo vya kuzalisha wachezaji wazuri.
Katika hatua nyingine wapenzi na washabiki wa timu ya Simba katika kusherehekea siku yao wameendesha harambee kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Kilago ambapo zaidi ya shilingi 100,000 zilipatikana.
Pia Mgeja alichangia kiasi cha shilingi 100,000 ili kuisaidia timu ya Nyanhembe Star inayoshiriki mashindano makubwa ya kitaifa ya Ndondo Cup yanayoendeshwa na Clouds FM ya jijini Dar es Salaam yanayotarajiwa kufanyika wilayani Kahama mkoani Shinyanga mwaka huu.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi