April 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Shinyanga kuchukulia hatua wanaobeza hatua za kujinga Corona

Na Anthony Ishengoma,Timesmajira Online, Shinyanga

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Philemon Sengati amesema atachukua hatua kwa watu ambao hawataki kuchukua tahadhari kujikinga na kuwakinga wengine dhidi ya ugonjwa wa Corona, hususan katika kipindi hiki ambacho wimbi la tatu la ugonjwa huo, linaonesha kuna wagonjwa katika Mkoa wa Shinyanga.

Dkt. Sengati amesema kuna wananchi na wadau ambao hawataki kuzingatia masharti yaliyowekwa na Wizara ya Afya, ili kujikinga na ugonjwa wa Corona na kuwataka watambue kuwa kuna sheria ya afya ya jamii ya mwaka 2009, inayotaka mtu ambaye anaambukiza wenzake kwa makusudi wakati kuna njia za kujikinga achukuliwe hatua.

Ameyasema hayo katika kikao cha siku moja cha Kamati ya Afya ya Mkoa, ambacho kilikaa kujadili namna bora ya kukabiliana na mlipuko wa wimbi la tatu la ugonjwa wa Corona katika Mkoa wa Shinyanga.

Mkuu huyo wa Mkoa, pia amewataka wadau kutoka asasi za kiraia na viongozi wa dini kushirikiana na serikali kutoa elimu kwa umma na kusisitiza wananchi, kuchukua hatua za kujikinga na ugonjwa huo.

Ameongeza kuwa, viongozi wa dini wakitumia sauti zao zenye mamlaka ya Mungu zinapokelewa kwa haraka, tofauti na makundi mengine katika jamii.

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Shinyanga, Dkt. John Luzila ameziomba asasi za kiraia mkoani hapa kuangalia upya maeneo ya ufadhili na kuziomba kuchangia mitungi ya gesi, ambayo ni gharama kubwa kutokana na mgonjwa mmoja wa Covid kutumia mitungi mitatu hadi mitano kwa siku, jambo ambalo ni kubwa kulinganisha mapato ya hospitali.

Dkt. Luzila amewaambia wajumbe wa kikao hicho kuwa, gharama ya mtungi mmoja ni sh. 50,000 na kwa uzoefu alionao mgonjwa mmoja anatumia sh. 150,000 hadi sh. 250,000 kwa siku na baadhi ya wagonjwa, wanakaa ndani ya oksijeni kwa takribani wiki moja au mbili na kuwa mzigo mkubwa kwa hospitali kugharimia.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Eudas Ndungile amesema kwa Mkoa wa Shinyanga ni muhimu kuchukua hatua kwa kuwa mkoa huo, una wageni wengi kutoka nchi jirani ambao wamekuwa wakipita katika Manispaa ya Kahama na kuongeza kuwa mkoa, unavuta watu kutoka maeneo mengine kufanya kazi katika migodi na kufanya biashara ya madini.

“Wafanyakazi wa migodini, wamekuwa wakifanya kazi kwa kubadilishana na kusafiri katika maeneo mengine ya nchi na hivyo kuchangia katika kuleta au kueneza ugonjwa huu katika migodi na kwa wakazi wengine maeneo jirani na migodi hiyo,” amesema.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala, Saimon Berege amewaambia wajumbe wa Kikao hicho kuwa tayari halmashauri yake, ina wagonjwa wa Covid na wengine vipimo vinapelekwa kwa Mkemia Mkuu kwa hatua za kiuchunguzi huku akiwataja wagonjwa hao kutoka Kakola, ambalo ni eneo jirani na mgodi mkubwa wa Bulyanhulu.

Berege ameishauri Serikali mkoani Shinyanga, kuwataka wananchi kuacha kwenda katika maeneo yenye mikusanyiko na kuanza kuchukua hatua kama ilivyo kwa nchi nyingine kwa kuzuia watu, kuendelea kujaa katika viwanja vya mpira kabla hali haijaanza kuwa mbaya zaidi.

Katika hatua nyingine, Shirika la World Vision Mkoa wa Shinyanga limetoa msaada wa vifaa tiba kwa ajili ya kusaidia kujikinga na kusaidia matibabu ya ugonjwa wa Corona yenye thamani ya sh. milioni 126.2 na kukabidhi vifaa hivyo kwa Halmashauri za Mkoa wa Shinyanga na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.