November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Shida ya maji Mombo kuwa historia

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Korogwe

MJI wa Mombo uliopo Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, utaondokana na shida ya maji baada ya Serikali kutenga kiasi cha zaidi ya bilioni 3.7 kwa ajili ya maboresho ya huduma ya maji kwenye mji huo.

Maboresho hayo yatakwenda sambamba na kubadilisha miundombinu yote chakavu ya maji ikiwemo mabomba, kusambaza mabomba katika mji wote wa Mombo, kujenga mtambo wa kisasa wa kutibu maji na kujenga Ofisi Ndogo ya Mamlaka ya Maji Safi ya Handeni Trunk Main (HTM) kwenye Mji wa Mombo.

Mkurugenzi Mtendaji wa HTM, Mhandisi Yohana Mgaza

Hayo yamesemwa Desemba 11, 2023 na Mkurugenzi Mtendaji wa HTM Mhandisi Yohana Mgaza alipokuwa anazungumza na Mwandishi wa Habari hizi ofisini kwake mjini Korogwe ambapo ameeleza kuwa HTM imepewa Miji ya Korogwe na Mombo kwa ajili ya kuboresha huduma za maji na usimamizi.

“Na safari hii sio kujenga vituo vya maji (vilula) tu kwenye mitaa ya Mombo, bali tutahakikisha maji yanafika na kuwekwa kwenye nyumba za watu,tunataka kuona maji yanawafikia wananchi pale walipo” amesema Mhandisi Mgaza.

Mhandisi Mgaza amesema, hata Baraza la Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mombo, ambapo yeye alihudhuria wiki iliyopita amewaeleza huduma ya maji ina gharama na ni lazima ilipiwe, hivyo ili kuleta ufanisi lazima wananchi walipie ambapo gharama ya ndoo ya maji ya lita 20 itauzwa kwa sh. 20 badala ya sh.8.

Tenki la maji lililopo Mji wa Mombo lenye ujazo wa lita 500,000

Mhandisi Mgaza amesema wapo kwenye hatua ya manunuzi ya kumpata Mkandarasi lakini kazi hiyo ya maboresho inatarajiwa kuanza Januari, mwakani.

Amesema HTM imepewa Mji wa Mombo kwa ajili ya kuboresha huduma na usimamizi kwani awali ilikuwa chini ya Mamlaka Ndogo ya Maji ambayo ilikuwa chini ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) lakini Septemba, mwaka huu ikahamishiwa chini ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na sasa ipo chini ya HTM.

Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Mamlaka ya Mji Mdogo Mombo wakiwa kwenye picha ya pamoja na wataalamu wa HTM mara baada ya kikao cha Baraza hilo.