Na Martha Fatael,Timesmajiraonline
MLIMA Kilimanjaro ni zaidi ya kivutio cha utalii. Ni chanzo cha maji, urithi wa taifa na nguzo ya maisha ya maelfu ya wananchi wanaouzunguka. Hata hivyo, licha ya kuwepo kwa sheria madhubuti za mazingira, uhalisia unaoonekana katika baadhi ya maeneo yanayozunguka mlima huo unaibua maswali mazito: kwa nini ulinzi wake unaendelea kudhoofika, na ni nani anayepaswa kuwajibika?
Uchunguzi huu unaangazia utekelezaji wa wajibu wa kisheria wa serikali za mitaa, hususan Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini, na kubaini sababu zinazoifanya sheria kubaki kwenye makaratasi huku mazingira yakizidi kuharibika.

Wajibu wa kisheria: mamlaka yapo, utekelezaji unasuasua
Kwa mujibu wa Kifungu cha 37(1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 (EMA), mamlaka za serikali za mitaa zina wajibu wa kusimamia na kulinda mazingira ndani ya maeneo yao. Vifungu vya 38 na 40 vinaelekeza wazi kuwa halmashauri zinapaswa kuandaa na kutekeleza mipango ya uhifadhi, kudhibiti matumizi holela ya ardhi na kuchukua hatua dhidi ya uharibifu wa mazingira.
Aidha, Kanuni za Usimamizi wa Mazingira zinazitaka mamlaka hizo kushirikisha jamii katika ulinzi wa misitu na vyanzo vya maji, kwa kutambua kuwa wananchi ni walinzi wa kwanza wa mazingira yao.
Licha ya mamlaka hayo ya kisheria, hali ilivyo sasa inaonyesha pengo kubwa kati ya matakwa ya sheria na utekelezaji wake katika maeneo yanayozunguka Mlima Kilimanjaro.
Hali halisi: migogoro ya ardhi, ukame na wananchi kutengwa
Katika Kata ya Kimochi, baadhi ya wakazi wanasema hawashirikishwi katika mipango ya uhifadhi wa mlima na misitu inayowazunguka. Elifuraha Mroki anasema ushiriki wa jamii hauonekani, licha ya wao kuishi karibu kabisa na maeneo yanayolindwa.

“Tunaambiwa tu ni marufuku kuingia msituni. Hatuna elimu wala mikakati ya pamoja ya kutunza huu mlima,” anasema Elifuraha.
Mkazi wa Marangu, Elienanga Mushi anasema ukosefu wa ushiriki huo umesababisha baadhi ya wananchi kuendelea na shughuli hatarishi kama ukataji miti na uchomaji moto msitu, si kwa kupenda, bali kwa kukosa mbadala wa kipato na usimamizi shirikishi.
Kwa upande wake, mkazi wa kata ya Kirua Vunjo Kusini, Gopali Mdunda anasema athari kubwa zaidi kwa sasa ni ukame na uhaba wa maji, hali inayozidi kuwaumiza wananchi wa kawaida.
Mikakati ipo, lakini iko wapi utekelezaji?
Uchunguzi unaonyesha kuwa nyaraka muhimu za uhifadhi, ikiwemo mipango ya matumizi ya ardhi na Environmental Action Plan, zinapaswa kuwepo katika ngazi ya halmashauri. Hata hivyo, jitihada za kupata maelezo kuhusu utekelezaji wa mipango hiyo katika maeneo yanayozunguka Mlima Kilimanjaro hazikuzaa majibu ya wazi.
Kutokuwepo kwa taarifa za wazi kuhusu lini mipango hiyo ilipitishwa, ilitekelezwa au kufanyiwa mapitio, kunazua maswali juu ya ufanisi wa usimamizi wa mazingira katika ngazi ya chini.
Bajeti ndogo na mazingira kutopewa kipaumbele
Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Moshi Vijijini, Peter Tungu, anakiri kuwa changamoto kubwa ni ufinyu wa bajeti na kuwa mapato ya halmashauri ni madogo, jambo linalofanya masuala ya mazingira kushindwa kupewa uzito unaostahili.
“Kwa mapato tuliyonayo, sekta ya mazingira mara nyingi haiwekwi mbele ikilinganishwa na mahitaji mengine,” anasema Tungu.
Hata hivyo, wataalamu wa sheria za mazingira wanasema hoja ya bajeti haiwezi kuwa kisingizio cha kutotekeleza wajibu wa kisheria. Kifungu cha 42 cha EMA 2004 kinazitaka mamlaka husika kuhakikisha mazingira yanalindwa kwa kutumia rasilimali zilizopo na mbinu mbadala, ikiwemo ushirikiano na jamii na wadau wengine.
Uongozi wa juu: kauli haikupatikana
Juhudi za kupata kauli ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Moshi Vijijini, Shedrack Mhagama, hazikufanikiwa. Ofisi ya halmashauri ilieleza kuwa alikuwa kwenye kikao katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Kutopatikana kwa kauli ya uongozi wa juu kunazidi kuacha maswali kuhusu hatua za kimkakati zinazochukuliwa kuhakikisha sheria za mazingira zinatekelezwa kikamilifu, hasa katika eneo nyeti kama Mlima Kilimanjaro.
Mtazamo wa wataalamu: tatizo si sheria, ni uwajibikaji
Akizungumza kuhusu hali hiyo, mwanasheria wa mazingira Adv. Dkt. Rehema Lema anasema Tanzania haina upungufu wa sheria, bali ina upungufu wa uwajibikaji katika utekelezaji.
“EMA 2004 ni sheria yenye meno. Tatizo ni kutotumika kwa vifungu vinavyowawajibisha viongozi na taasisi zinazoshindwa kutekeleza majukumu yao,” anasema Dkt. Lema.
Anarejea Kifungu cha 191 cha EMA, kinachoruhusu kuchukuliwa hatua za kisheria dhidi ya mamlaka au viongozi wanaoshindwa kusimamia mazingira wanayopaswa kulinda.
Mtaalamu wa uhifadhi na mabadiliko ya tabianchi, Dkt. Deus Mushi, anasisitiza kuwa bila ushiriki wa jamii, ulinzi wa Mlima Kilimanjaro hauwezi kufanikiwa.
“Jamii zinazozunguka mlima ndizo walinzi wa kwanza. Kuwatenga ni kujitengenezea mazingira ya kushindwa,” anasema.
Athari kwa jamii na uchumi wa utalii
Mwenyekiti wa Kijiji cha Yamu Makaa, Edward Kimambo, anakiri kuwa hali ya mazingira imeendelea kuwa ngumu. Anasema kijiji hicho hakijapata miche ya miti kwa muda mrefu, huku ukame ukiongezeka na kusababisha mgawo mkali wa maji.
“Kuna nyakati maji yanakosekana kwa siku kadhaa, wananchi wanalazimika kununua maji,” anasema Kimambo.
Hali hii si tishio kwa jamii pekee, bali pia kwa sekta ya utalii inayotegemea Mlima Kilimanjaro kama nembo ya mazingira salama na yanayovutia.
Nani awajibike, na nini kifanyike?
Kinachojitokeza katika uchunguzi huu si ukosefu wa sheria, bali pengo kubwa kati ya wajibu wa kisheria na uhalisia wa utekelezaji katika ngazi ya serikali za mitaa. Kwa mujibu wa EMA 2004, kushindwa kutekeleza majukumu ya mazingira si suala la hiari, bali ni kosa la kiutawala linalopaswa kuwajibishwa.
Wataalamu wanashauri serikali kuu kuziimarisha kifedha na kitaasisi halmashauri zinazozunguka Mlima Kilimanjaro, huku zikilazimishwa kuweka wazi mipango, bajeti na hatua zinazochukuliwa kulinda mazingira. Vilevile, jamii zinapaswa kushirikishwa kikamilifu kama washirika, si watazamaji.
Hitimisho
Makala hii inaonyesha kuwa hatari inayoukabili Mlima Kilimanjaro haipo kwenye upungufu wa sheria, bali kwenye udhaifu wa uwajibikaji wa ngazi ya chini. Bila hatua za makusudi na ufuatiliaji wa karibu, mlima huo utaendelea kuwa kwenye hatari, licha ya kuwepo kwa sheria zinazolenga kuilinda.
Makala hii ni sehemu ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa sheria za mazingira katika maeneo yanayozunguka Mlima Kilimanjaro.


More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina