November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sheria ya mtoto ikisimamiwa,watoto mitaani watapungia

Na Suleiman Abeid, TimesMajira Online 

MOJA ya changamoto inayoendelea kuikabili nchi yetu ni suala la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi ama twaweza kusema “mazingira magumu” ambapo kwa wengi wetu tumezoea kuwaita watoto wa “mitaani.”

Tunaposema watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi au “watoto wa mitaani” kama ilivyozoeleka kwa wengi tunamaanisha ni watoto waliokosa makazi bora, huduma za matibabu, malazi na mavazi kutoka kwa wazazi au walezi wao na hivyo kutokuwa na eneo maalumu la kuishi. 

Changamoto hii kwa sasa imeenea katika mikoa yote nchini hapa hasa maeneo ya mijini ambako watoto hao huzagaa mitaani kila siku wakihangaika kujitafutia maisha ikiwemo kupata fedha za kujikimu kimaisha na kulala katika maeneo yasiyo rafiki.

Serikali iliwahi kukiri kuwepo la ongezeko la watoto wanaoishi mitaani na kufanya kazi ndogondogo ikiwemo uokotaji wa vyuma chakavu na uoshaji magari hasa katika miji mikubwa nchini.

Ambapo takwimu zikionesha Jiji la Dar es salaam linaongoza kwa asilimia 28 ya watoto hao ikifuatiwa na miji mingine kama Mwanza, Dodoma na Tanga.

Kwa mujibu wa sheria nchini  hapa na zile za kimataifa ikiwemo Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto (CRC) wa mwaka 1989 mtoto chini ya miaka 18 kufanyishwa kazi ni kosa huku  Mkataba wa CRC unawataka watu wazima kulinda maslahi ya watoto na Serikali kulinda haki zao kama vile elimu, afya na mengineyo.

Watoto hawa kiuhalisia hawastahili kuachwa kuendelea kuishi katika hali waliyonayo hivi sasa kama wanavyoonekana katika maeneo mengi hapa nchini maana ipo hatari ya kuwaambukiza wengine ambao wataona maisha wanayoishi ni hali ya kawaida kwa watoto wa kitanzania.

Mara nyingi mamlaka za Serikali kuanzia ngazi za mitaa hadi taifa hujadili suala la watoto hawa kwa ajili ya  kuona jinsi gani watasaidiwa na wakati mwingine inapotokea “mfadhili” kujitokeza kutaka kuwasaidia, basi hufanyika zoezi la zimamoto la kuwakusanya na kuwapatia misaada iliyotolewa na kisha hurejea walikotoka.

Pamoja na Serikali kutoa matamko ya mara kwa mara yanayoonesha dhamira ya kutaka kuwasaidia watoto hawa, hasa wale wanaoishi mitaani na kulala katika maeneo hatarishi bado utekelezaji halisi wa kusaidiwa kwao hakuonekani.

Ushahidi wa kutoonekana kwa msaada wa Serikali kwa watoto hawa upo wazi katika Bajeti za Halmashauri nyingi hapa nchini ambapo hata pale panapotengwa fedha kidogo basi huwekwa kwenye kapu la jumla la Idara ya Maendeleo ya Jamii na sehemu kubwa hutarajiwa misaada kutoka kwa wafadhili (NGOs).

Mbali ya kusaidiwa lakini pia mamlaka hizo za Serikali za Mitaa hazina mipango yoyote endelevu ya angalau kuwajengea makazi maalumu yatakayotumika kuwalea ambayo yanaweza kuwa ni fursa muhimu kwao ikiwemo kupata elimu na kujifunza mafunzo mbalimbali ya ufundi kwa waliovuka umri wa kusoma.

Tafiti zilizowahi kutolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) zinaonesha nusu ya watoto duniani wanaishi katika hali ya ufukara ambayo ni sawa na watoto bilioni 1.1.

Pia utafiti wa makadirio ya ulimwengu ya watoto katika umaskini wa kifedha (2020) inaonesha kuwa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, theluthi mbili ya watoto wanaishi katika kaya zinazotumia chini ya dola 1.90 kwa siku.

Miongoni mwa changamoto zinazowakabili watoto hawa ni suala la ukosefu wa huduma za uhakika za matibabu pindi wanapopatwa na ugonjwa wowote na hivyo hujiuguza wao wenyewe kwa shida na wakati mwingine baadhi yao hupoteza maisha kutokana na maradhi yanayowapata hii ni kwa vile hawapati tiba za uhakika.

Wakati dunia ilipokumbwa na janga la gonjwa hatari la UVIKO-19, hakuna aliyewakumbuka watoto hawa kwa kuwapa angalao elimu ya jinsi ya kujikinga na gonjwa hilo hatari japokuwa takwimu zilionesha ugonjwa huo haukuwa ukiwathiri sana watoto wenye umri mdogo.

Pamoja na kwamba tafiti zilionesha watoto hawaathiriwi na janga la UVIKO-19, lakini palikuwa na uwezekano mkubwa wa wao kuugua ugonjwa huo na kuusambaza hata kwa watu wazima hivyo na wao pia walipaswa kukumbukwa kwa kundi lao kupatiwa elimu ya kujikinga na janga hilo.

Mbali ya changamoto ya maradhi lakini athari nyingine ya kuongezeka kwa kundi la watoto wa mitaani ni kuibuka kwa magenge ya kiuhalifu, mara ngapi katika baadhi ya miji mikuu tumekuwa tukisikia watu kuvamiwa na kuporwa mali zao na makundi ya watoto wanaojiita “Panyaroad?”

Ukichunguza kwa undani utabaini wengi wa watoto wanaojiunga na makundi haya wanatokea kwenye kundi la watoto wa mitaani, ambako huishi bila mafunzo yoyote ya tabia njema aidha kutoka kwa wazazi ama walezi wao na hivyo kujikuta katika makuzi yao wanajichunga kama kuku wa kienyeji.

Katika moja ya taarifa ambazo zimetolewa hivi karibuni na Ofisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Shinyanga Lydia Kwesigabo, anasema mpaka hivi sasa mkoa huo unakadiriwa kuwa na watoto wa mitaani wapatao 612 huku wanaoishi kwenye mazingira hatarishi  99,939.

“Kwa takwimu hizi tunaona wazi kuna kila sababu ya Serikali hivi sasa kuja na mikakati madhubuti itakayowezesha kuwasaidia watoto hawa na kutafiti kwa kina nini chanzo cha wao kukimbia kwa wazazi ama walezi wao……tatizo hilo la watoto wa mitaani lisipo dhibitiwa mapema linaweza kutokea tatizo kubwa hapo baadae mfano Taifa linaweza kuwa na wimbi kubwa la vibaka wa mitaani,”anasema Kwesigabo na kuongeza kuwa 

“Uwepo wa watoto hawa katika miji yetu, ukichunguza kwa umakini utaona chanzo chake ni uwepo wa migogoro ya ndoa, umasikini wa kipato na malezi duni kutoka kwa wazazi ama walezi na wengi hutoroka nyumbani kwao baada ya kujifunza utumiaji wa madawa ya kulevya wakiwa na umri mdogo.”

Katika moja ya mikakati ya kukabiliana na wimbi ongezeko la watoto hawa, moja ya taasisi iliyopo mkoani Shinyanga ya Nancy Foundation imeamua kushirikiana na vyombo vya Serikali mkoani humo kuona jinsi gani watawaondoa watoto hao  mitaani.

Hii inaweza kuwa moja ya njia sahihi ya kukabiliana na wimbi hili iwapo tu pindi watakapokusanywa na kuondolewa mitaani watatafutiwa fursa mbalimbali ikiwemo kuwarejesha shule kwa waliokimbia masomo na kuwafundisha elimu ya ufundi itakayowasaidia kuweza kujiajiri wenyewe baada ya kuhitimu mafunzo yao.

Mkurugenzi wa Taasisi Nancy Foundation, Ezra Manjerenga amenukuliwa hivi karibuni akisema wameanza kuweka utaratibu utakaowawezesha kuwakusanya na kuwaondoa mitaani watoto wote wanaoishi kwenye mazingira hatarishi kwa lengo la kuwakutanisha na wazazi wao pamoja na kuona namna ya jinsi ya kuwasaidia pamoja na kuwapatia elimu.

Ambapo Anasema kuwa kila sababu ya kuangalia ni jinsi gani tabia hii ya watoto kukimbilia mitaani inakomeshwa katika miji yetu mingi hapa nchini, maana tunaona wazi kuwaacha waendelee kuzagaa mitaani kuna athari kubwa hapo baadae kutokana na wao kukosa mwelekeo wa maisha na hivyo kujiingiza kwenye makundi ya kiuhalifu,”.

Anasema kuendelea kuibuka kwa makundi ya watoto wa mitaani katika miji mingi kunachangiwa na Serikali na jamii yenyewe kutosimamia kikamilifu Sheria za Haki na ulinzi wa mtoto zilizopo hapa nchini ambazo iwapo zingezingatiwa kila ngazi kuanzia ngazi ya kijiji, kata, wilaya na hata mkoa watoto hawa wangeweza kutunzwa vyema. (Rejea Sheria za Haki ya Mtoto 2009).

Naamini iwapo tutasimamia vyema sheria zetu zote zinazohusu ulinzi wa mtoto zilizopo hapa nchini pamoja na kutekeleza kikamilifu mikataba ya kimataifa inayohusu ulinzi wa mtoto ambayo nchi yetu imeridhia tunaweza kupunguza kwa kiasi fulani kama siyo kukomesha kabisa.

Mfano tukitupia macho katika Sheria ya Haki za Mtoto za mwaka 2009 Sura ya 12 inayozungumzia huduma ya msaada kwa mtoto kutoka mamlaka za Serikali za mtaa inaelekeza njia mbalimbali za kuweza kumlinda mtoto hasa wale waliotelekezwa.

Mfano ni Ibara ya kwanza katika sura hiyo ya 12 inayoeleza, nanukuu; “….Mamlaka ya Serikali ya Mtaa itakuwa na wajibu wa kulinda na kukuza ustawi wa mtoto katika eneo la mamlaka hiyo,” mwisho wa kunukuu.

Sasa tujiulize ni Serikali ngapi za mitaa zenye mpango mkakati wa kuhakikisha zinasimama kidete na kutekeleza Sheria hiyo? Tunaweza kuona wenyewe watoto wengi wanaozagaa hovyo mitaani wanaishi katika makazi yetu yenye mamlaka hizo za Serikali je, kuna hatua zozote zinazochukuliwa na viongozi wake za kuwasaidia watoto hao?

Vilevile tukitupia macho kwenye Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto (CRC) wa mwaka 1989 tunaona pia katika Ibara yake ya nne ikizungumzia kuhusu Serikali kuzitekeleza na kuzilinda haki zote za mtoto, kama inavyoeleza, nanukuu;-

“Serikali zote zilizoridhia mkataba huu zina wajibu wa kuhakikisha haki zote za watoto zinalindwa, zinatekelezwa na kuthaminiwa na kila mtu. Na ili kufanikisha hili ni lazima kupima utendaji wa sekta zote ili kuona kama zinatekeleza haki hizi.”

“Serikali pia ina wajibu wa kuzisaidia familia ili kufanikisha ulindaji na ukuzaji wa haki za watoto hata kwa kuweka sheria nzuri na maadili yanayokubalika,” mwisho wa kunukuu. Sasa kila mmoja anapaswa anao wajibu wa kutekeleza sheria hizi ili kuwanusuru watoto wetu wanaozagaa hovyo katika maeneo mengi ya miji yetu.

Naamini iwapo tutaamua tunaweza, ifike wakati tujiulize iweje kila mwaka tunaimba wimbo ule ule wa kuwasaidia watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi lakini hakuna badiliko lolote linalotokea na badala yake kumekuwepo na ongezeko kubwa la watoto hawa katika mitaa yetu, inaonesha wazi matendo yetu ni ya “nadharia” zaidi kuliko “vitendo” sasa tuamue kuthubutu.