AJALI nyingi zinatokea barabarani husababishwa na sababu mbalimbali ikiwemo makosa ya kibinadamu,ufinyu wa barabara, mwendokasi na uzembe wa madereva hasa wengi wao kukosa elimu ya kutosha kuhusiana na sheria za barabarani.
Nchi za Afrika Mashariki zina sheria za barabarani ambazo katika maandishi huonekana nzuri,japo wadau wa usafirishaji wakisema sheria hizo sio kali kama ilivyo katika nchi nyingine.
Zipo nchi zenye sheria kali kidogo hasa kwa madereva wa mabasi,ikiwemo nchi ya Angola na Rwanda huwezi kukuta madereva wakifanya uzembe wanapokuwa wakiendesha magari yao.
Kwa nchi ya Tanzania bado sheria ya mwaka 1973 inahitaji kufanyiwa maboresho kwa umakini zaidi kuhakikisha madereva wanabanwa wawapo barabarani kwa lengo la kupunguza ajali.
Kutokana na sheria hiyo kutowabana sana bado madereva wamekuwa wakiendesha vyombo vyao vya moto huku wakiongea na simu hali inayowafanya kuondoa umakini wa barabarani.
Na hii yote inatokea kwa sababu ya kutotii sheria na kanuni za barabarani, hali inayowafanya kuipuuza na kufanya vitu ambavyo ni hatari kwa usalama wa barabarani.
Irene Msellem Afisa Utawala wa Taasisi ya Mabalozi wa Usalama Barabarani Tanzania(RSA Tanzania) anasema dereva anapokuwa anatumia simu wakati anaendesha gari mara nyingi umakini upotea katika kuendesha gari.
Anasema teknolojia ya simu ni nzuri lakini inamadhara kwa watumiaji kama madereva wasipokuwa makini.
“Kuongea na simu pindi dereva anapokuwa anaendesha chombo cha moto hupoteza kabisa umakini na utegemea anaongea na simu ya aina gani kwani wakati mwingine hupokea taarifa ambayo si nzuri na matokeo yake uja kuwa mabaya,”anasema.
Anasema madereva wa magari ya abiria wanaopopigiwa simu ni vema wakawapa wasaidizi wao wapokee simu zao na sio wao waongee nazo kwani inaweza ikawa hatari pindi anapopokea simu na kupewa taarifa ambazo zio nzuri na kupelekea kupata mshtuko.
“Ni vema dereva wa basi akampa kondakta wake simu ampokelee anapopigiwa na madereva wa magari madogo ni vema akapaki gari pembeni kisha aongee na simu na sio kuendesha gari huku akiwa anaongea na simu,’’anasema Msellem.
Anasema wao kama mabalozi wa usalama barabarani wanatamani kuona madereva wa magari haya ya abiria wasitumie kabisa simu wanapokuwa wanaendesha magari yao na hawa madereva wenye magari madogo watumie lakini wahakikishe wanapaki pembeni.
Msellem anasema katika sheria kuna vitu vitatu faini,onyo na kifungo katika kifungo lazma dereva apelekwe mahakamani…suala la kutoa kwa onyo ni vema ishuke kwa maaskari wote wa usalama barabarani na sio kutolewa na RTO pekee .
Anasema sheria inasema onyo inatolewa na masharti tu hivyo kwa sasa inabidi sheria iongezewe na kutolewa kwa maaskari wote.
“Huwa tunatembea katika maeneo mbalimbali na kuwasihi madereva kama simu hazina umuhimu wakati wa kuendesha gari waache wasitumie ili kusaidia kupunguza ajali za barabarani,”anasema.
Pia anasema sheria itambue kuwa ni kosa kwa dereva anapoongea na simu wakati akiwa anaendesha gari.
“Tunatamani sana ifike mahali sheria hii ije kuheshimiwa kama ile ya dereva kutokunywa pombe tutazidi kupiga hatua juu ya kupunguza ajali za barabarani,”anasema.
Kwa Upande wake Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara (LATRA),Johansen Kahatano, anasema unapoendesha gari unakiona kitu unakitafsiri visivyo hivyo ni lazima kuwa makini katika kuendesha gari.
Anasema unapoongea na simu kwenye gari dereva anashindwa kutoa maamuzi au majibu sawasawa kutokana na wakati huo anakuwa hayupo makini kwa kuendesha gari.
Pia anasema inamfanya dereva kushindwa kuendesha kwa mikono miwili kwani mkono mmoja unakuwa umeshika simu na mwingine mskani hivyo ikitokea dharura dereva anashindwa kuzuia na kusababisha ajali.
“Mtu anaendesha gari lazima awe anafikiria nini anachoifanya kwa wakati huo hauwezi kufanya vitu viwili kwa wakati mmoja kwani unaweza kupata ajali kutokana na kushindwa kuzuia dharura inayoweza kujitokeza kwa wakati huo,”anasema Kahatano.
Naye Mwanasheria wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini,Afande Deus Sokoni ,anasema baada ya sheria itakapofanyiwa maboresho haitaruhusiwa kwa mtu yeyote kutumia simu au ipad anapokuwa anaendesha gari.
“Tumependekeza katika sheria ya mwaka 1973 inayofanyiwa marekebisho na hii itasaidia kufanyiwa marekebisho kuhakikisha dereva anaendesha gari akiwa anaongea na simu anachukulia hatua,”anasema.
Anasema kwa sasa hivi hakuna faini yeyote kwa mtu anapokutwa anaongea na simu wakati akiendesha gari zaidi ya kushauriwa kuacha kutumia simu wakati akiendesha gari.
“Kwa sasa tunapomkuta mtu anaendesha gari huku akiongea na simu mara nyingi tunamshari na kumwambia madhara yake kwani sheria iliyopo haina adhabu yeyote juu ya kosa hilo,”anasema Sokoni.
Aidha Sokoni anasema hali ya ajali za barabara kwa sasa zimeweza kupungua kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma .
More Stories
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini
Rais Dk. Samia alivyowezesha Tanzania kuwa kinara usambazaji umeme Afrika