Na Penina Malundo,Timesmajira
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025 imefanikiwa utungwaji wa sheria takribani 68 huku jumla ya sheria 297 zimefanyiwa marekebisho kutokana na mabadiliko ya kimazingira na kuwepo kwa mahitaji mapya.
Pia imesema katika kipindi hicho Ofisi hiyo imeweza kutafsiri sheria 433 kwa lugha ya kiswahili huku nyingine zilizotungwa kwa sasa zimetumia lugha ya kiswahili na kutafsiriwa kwa lugha ya Kiingereza.
Hayo yamebainisha jana Septemba 11, 2025 Mkoani Dodoma na Mwandishi Mkuu wa Sheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Onorius Njole katika kikao kazi kati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wahariri wa vyombo vya habari kilichofanyika ukumbi wa Mkemia Mkuu wa Serikali Dodoma.
“Kama mlivyoona tunazo sheria 446 ila zilizotafsiriwa ni 443 hiyo ni kwa sababu zingine zilishatungwa kwa kiswahili na zimewekwa katika lugha ya Kingereza pia, hata hivyo tumefanya urekebu wa sheria zote 446 na kutengeneza sheria ndogo 5,708,” amesema

Aidha amesema baadhi ya sheria zilizofanyiwa mabadiliko makubwa ni pamoja na Sheria ya Usuluhishi ambayo imefanyiwa marekebisho hayo kwa lengo la kuimarisha mfumo wa utatuzi wa migogoro nje ya mahakama.
Amesema mwaka 2022 walifanya marekebisho ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kwa kuweka utaratibu wa matumizi sahihi ya taarifa binafsi za watu.

“Mwaka 2021 tulifanya marekebisho ya sheria mbalimbali kwa lugha ya sheria na mahakama kwa kiswahili, Mwaka 2024 Sheria ya Uchaguzi na Vyama vya Siasa nayo ilirekebishwa pamoja na Sheria ya Ulinzi wa mtoto ili kuimarisha ulinzi wa mtoto katika Nyanja mbalimbali ikiwemo ajira, utoaji wa ushahidi pamoja na makosa ya kimasai,” amesema
Amesema Ofisi yao inamatarajio ya kuongeza kasi ya ubora na ufanisi katika utoaji wa huduma za uandishi wa sheria,kuimarika kwa taswira na kujenga imani katika mfumo wa sheria na kuongezeka kwa ushirikishwaji wa wadau.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi