October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sherehe za ubingwa Simba kufanyikia Ruagwa Julai 8, TFF yaonya

Na Mwandishi Wetu

BAADA ya kutwaa ubingwa wa msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) na wa tatu mfululizo huku wakiwa wamebakiza mechi sita, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeweka wazi kuwa, sherehe za kukabidhi kombe kwa mabingwa hao zitafanyika Ruangwa mkoani, Lindi Julai 8, 2020.

Simba ilitwaa ubingwa huo jijini Mbeya katika mchezo wao wa Juni 28 dhidi ya Tanzania Prisons uliochezwa kwenye uwanja wa Sokoine ambao ulimalizika kwa suluhu ya bila kufungana.

Licha ya sare hiyo lakini Simba ilifanikiwa kufikisha pointi 79 ambazo hatitoweza kufikiwa na timu yoyote katika Ligi hata ikitokea wakapoteza mechi zao zote zilizosalia.

Baada ya kutwaa ubingwa huo sasa vita kubwa ipo kwenye nafasi ya pili ambayo inawaniwa na Yanga wenye pointi 60 na Azam waliofikisha pointi 59 zote zikiwa zimecheza mechi 32.

Itakumbukwa kuwa, mara baada ya kutwaa ubingwa huo, Simba kupitia kwa msemaji wake, Haji Manara waliamua kuahirisha sherehe za ubingwa huo kutokana na umuhimu wa mchezo wao wa jana usiku dhidi ya Azam na baada ya kumalizana na wapinzani wao ndio wataanza kuandaa rasmi sherehe hizo za ubingwa.

Amesema, kwa sasa kipaumbele chao kipo kwenye mchezo huo kwani wanakutana na timu ambayo wanaiheshimu sana kutokana na ubora mkubwa na uwezo walionao.

Kwa mujibu wa TPLB, shughuli hiyo itafanyika kwenye uwanja wa Majaliwa mara baada ya kumalizika kwa mchezo namba 340 kati ya wenyeji
Namungo FC dhidi ya Simba.

Baada ya taarifa hiyo, mashabiki wa klabu ya Simba wamesema kuwa, wanachokisubiri ni maelekezo kutoka kwa viongozi wao ni namna gani sherehe hizo zitafanyika kwani licha ya TPLB kutangaza kufanyikia Ruangwa lakini wao wamejipanga kufanya shehere za kufuru hapa jijini.

Katika hatua nyingine TPLB, imezikumbusha klabu zote zinazoshiriki Ligi Kuu (VPL), Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na Daraja la Pili (SDL) kuzingatia kanuni ya 30.

Kanuni hiyo inasema kuwa, endapo timu yoyote itabainika kuwa imepanga kwa namna yoyote ile matokeo ya mchezo wowote waliocheza kwa madhumuni yoyote yale zitachukuliwa hatua kali ikiwemo kusimamishwa mechi na kufungiwa kushiriki shughuli yoyote ya mpira wa miguu kwa kipindi kisichopungua miaka 10 na faini isiyopungua sh. 10,000,000 na katika shauri linalovuruga hadhi ya mpira wa miguu, mhusika atafungiwa maisha.

Lakini pia, ikiwa mchezaji au kiongozi atajishughulisha katika kushawishi upangaji matokeo kama ilivyo katika kanuni ya 30 (1a), klabu au Mkoa ambao mchezaji au kiongozi anatoka utapigwa faini.

“Katika makosa mazito itaadhibiwa kwa kuondolewa kwenye Ligi, kushushwa Daraja, kupunguziwa pointi na kurudisha zawadi, hivyo tunazikumbusha timu kuzingatia haya kwani tupo macho kuelekea kwenye michezo ya kumalizia Ligi msimu wa 2019/2020,” imesema taarifa hiyo.

Hata hivyo Bodi ya Ligi imesema kuwa, imejipanga vilivyo kupeleka wasimamizi kwenye michezo yote iliyobaki ili kuhakikisha mechi zote zinachezwa kwa kuzingatia kanuni na sheria za mpira wa miguu.