March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Shemdoe awataka madiwani kutoa ushirikiano kwa watendaji

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Lushoto

WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Profesa Riziki Shemdoe amewataka madiwani nchini kushirikiana na watendaji na wataalamu kwenye halmashauri  ili kwa pamoja waweze kutekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi.

Amesema ukiacha Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango (FUM) ambayo inakutana kila mwezi, vikao vya kamati nyingine ikiwemo Baraza la Madiwani, wao wanakutana kila baada ya miezi mitatu, lakini watendaji wao wanafanya kazi kila siku, hivyo ni muhimu kuwapa nguvu kwa kuwapa ushirikiano.

Amesema hayo Desemba 5, 2025 alipozungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, ambapo kikao hicho kilikwenda sambamba na kumchagua Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti, pamoja na Kamati za Kudumu za Halmashauri hiyo.

Prof.Shemdoe ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga, amesema anatamani kuona halmashauri hiyo inakuwa ya mfano katika utendaji ikiwemo ukusanyaji mzuri wa mapato ili kumjengea yeye taswira nzuri nchini, kwani halmashauri hiyo ikifanya vibaya, na yeye hataaminika maeneo mengine.

“Madiwani wenzangu, ili tuwe na halmashauri inayong’ara ni lazima tuwapende hawa ndugu zetu wataalamu. Hawa wataalamu bila kufanya kazi, hata sisi hatutafanya kazi. Sisi tunakuja hapa mara moja baada ya miezi mitatu, lakini hawa wataalamu ndiyo wapo kila siku. Tukiwachanganya hawa ni sawa tumejichanganya wenyewe, na ile tabasamu tunayoitegemea ifike kwa wananchi, haitafika.

“Hivyo, nawaomba sana ndugu zangu, wazee wangu, mama zangu, kaka zangu, dada zangu, wadogo zangu, tukiwa wamoja hata halmashauri inakuwa na mafanikio sababu halmashauri haiwezi kuwa halmashauri kama haina Mwenyekiti, kama haina madiwani, na kama haina wataalamu. Kwa hiyo sisi wote tukishakuwa kitu kimoja, hakika halmashauri hii itang’ara. Na mjue kwa sasa hivi, halmashauri ambayo itakuwa inaangaliwa sana ni hii… si ndiyo imetoa Waziri wa TAMISEMI, hivyo na mimi mmenipa mzigo, mkikorofisha, kokote nitakapokwenda nikitaka kuzungumza, hawatanielewa, hivyo ninyi ndiyo kioo changu” amesema Prof.Shemdoe.

Prof.Shemdoe aliwashukuru wananchi wa Jimbo la Lushoto kwa kuweza kumchagua kwa kumpa kura nyingi, na kuwa Mbunge wa jimbo hilo. Pia amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumpa wizara hiyo yenye shughuli nyingi.

Akizungumza kwenye baraza hilo mara baada ya kuchaguliwa, ambapo wajumbe wote 45 walimpa kura za ndiyo, na wala hakuna kura iliyoharibika, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Whitney Mwizagi amesema ili kufanya kazi kwa weledi, anahitaji ushirikiano kutoka kwa madiwani na watendaji wa halmashauri, huku Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Athuman Kingazi akiahidi kumsaidia vema Mwenyekiti, na kutaka umoja kwenye halmashauri hiyo kati ya madiwani na watumishi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Dkt. Ikupa Mwasyoge aliwapongeza na kuwakaribisha madiwani hao, na kuomba ushirikiano ili kuweza kutekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi kwenye kata zao.