Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Lushoto
MBUNGE wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga (CCM) Shaaban Shekilindi maarufu Bosnia amemaliza changamoto ya maji katika baadhi ya vitongoji vya Mji wa Lushoto kwa kununua mabomba ya maji (rola) ili wananchi wa vitongoji hivyo waweze kupata maji ya bomba.
Shekilindi alitekeleza ahadi hiyo ambayo iliahidiwa zaidi ya miaka 20 iliyopita kwa wabunge waliomtangulia, lakini kutokana na umuhimu wa wananchi wa vitongoji hivyo vya Dochi eneo la Shume- Jabali na Chake Chake eneo la Gagerstal, aliamua kutoa fedha zake za mfukoni ili kununua rola hizo.
Akizungumza Aprili Mosi, 2023 kwa nyakati tofauti na wananchi katika vitongoji hivyo kwenye hafla ya kukabidhi rola hizo, Shekilindi alisema changamoto ya maji kwenye vitongoji hivyo aliikuta kwenye makabrasha kama ahadi kutoka kwa watangulizi wake, lakini yeye ameamua kuitekeleza.
Shekilindi alisema kabla ya kupeleka mabomba hayo, eneo la Shume- Jabali barabara zake zilikuwa hazijawahi kuchongwa na greda tangu nchi kupata Uhuru, lakini kwa jitihada zake aliweza kupeleka greda na barabara hizo zikachongwa, sasa anajiandaa kuchonga barabara ambayo itaunganisha Shume- Jabali kwenda Kata ya Kwemashai.
Alisema, pia Shume- Jabali ilikuwa haijawahi kuwa na umeme tangu Uhuru, lakini jitihada zake zimewezesha eneo hilo kupata umeme, na sasa hivi unawaka. Hivyo mahitaji muhimu matatu ya wananchi wa Shume- Jabali yaani maji, barabara na umeme yamepatiwa ufumbuzi.
“Nilikuta suala la maji ni ahadi zilizotolewa na watangulizi wangu, lakini nikaamua kufanyia kazi, na nimeweza kutekeleza ahadi hiyo kwa kuleta rola tano ili mkishirikiana na RUWASA (Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira) muweze kuchimba mtaro kutoka kwenye chanzo hadi hapa, na mimi nitaongeza kwa kujenga kituo cha maji (kilula).
“Nimeweza kushughulikia changamoto zenu kubwa tatu ambazo ni maji, umeme na barabara. Wenyewe ni mashahidi, tangu Uhuru, barabara zenu zilikuwa hazijawahi kuchongwa na greda, lakini niliweza kupambana na kuleta greda likachonga barabara zenu. Sasa nipo kwenye jitihada za kuhakikisha barabara hii ya Shume- Jabali inachongwa na kuunganishwa na Kata ya Kwemashai. Hata umeme mmepata, na hizo ni jitihada zangu za kutimiza ahadi zangu kwenu” alisema Shekilindi.
Shekilindi akiwa Kitongoji cha Chake Chake eneo la Gagerstal, pamoja na wao kuwapelekea rola tano kwa ajili ya kupata maji eneo hilo, pia ameahidi kuwawekea kilula cha maji, na kujengewa daraja dogo kwenye eneo hilo ili iwe rahisi kwa ajili ya usafiri wa magari, pikipiki na kwa waenda kwa miguu. Pia aliahidi kutoa mifuko ya saruji 10 kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya CCM Tawi la Gagerstal.
Kabla ya kwenda kutoa rola 10 zenye thamani ya sh. milioni 1,260,000 kwa fedha zake za mfukoni maeneo ya Shume- Jabali na Gagerstal, Shekilindi alipita kukagua ujenzi wa choo cha matundu sita Shule ya Msingi Kitopeni iliyopo Lushoto mjini, ambapo alitoa mifuko ya saruji 20 yenye thamani ya sh. 310,000.
Naye Fundi wa RUWASA Wilaya ya Lushoto Charles Ligola ambaye alikuwa ameambatana na Mbunge, aliahidi kushirikiana na wananchi wa Shume- Jabali na Gagerstal kuhakikisha maji yanafika kwenye vitongoji hivyo kutoka kwenye chanzo kinachotunzwa na Taasisi ya Montessori chini ya Kanisa Katoliki, huku akiwaeleza wananchi hao kuwa lazima walipie maji ili kufanya miradi ya maji kuwa endelevu.
More Stories
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito