June 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Shekhe Mavumbi ahamasisha waislamu kupiga kura

Na Allan Kitwe, Tabora

WAUMINI wa dini ya kiislamu Mkoani Tabora wametakiwa kujitokeza kwa wingi kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu ili kuchagua madiwani, wabunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wito huo umetolewa leo na Shekhe wa Mkoa wa Tabora Al haj Ibrahim Mavumbi alipokuwa akitoa ujumbe wa sikukuu ya al adha kwa waumini wa dini hiyo kwenye Ibada ya swala ya eid iliyofanyika katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Amesema kuwa kupiga kura ni ibada inayompendeza Mwenyezi Mungu, hivyo kila muislamu na asiye muislamu ana haki ya kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo ili kutimiza haki yake ya msingi.

‘Serikali inawekwa na wanadamu, lakini anayechagua viongozi ni Mwenyezi Mungu mwenyewe, jukumu letu ni kujitokeza kupiga kura, nawaombeni tujitokeze kwa wingi mwaka huu’, amesema.

Shekhe Mavumbi amewataka kutokatishwa tamaa na maneno ya baadhi ya wanasiasa ikiwemo maneno ya uchochezi dhidi ya viongozi wa serikali kwa kuwa hayajengi bali yanachochea uvunjifu wa amani.

Amesisitiza kuwa ibada ya swala ya al adha ni ibada muhimu sana kwa kuwa inawasogeza waumini karibu zaidi na Mwenyezi Mungu, hii sio siku ya kufanya mambo machafu mbele za allah, kufanya hivyo ni kuasi mbele za Mungu.

Katibu wa Umoja wa Maimamu Tanzania (UMATA) Kanda ya Magharibi Shekhe Swalehe Masudi ameeleza kuwa sikukuu hii ni maalumu kwa ajili ya kuchinja, hivyo akatoa wito kwa kila muislamu kushiriki ibada hiyo kikamilifu.

‘Ibada ya kuchinja ni utekelezaji agizo la Mwenyezi Mungu kwa Nabii wake Ibrahimu alipoambiwa atoe sadaya ya mwanawe wa pekee kwa kumchinja, akatii agizo la Mwenyezi Mungu’, alisema.

Aidha katika ibada hiyo Shekhe wa Mkoa amemwombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake wote na kuiombea nchi amani na utulivu kuelekea uchaguzi mkuu mwaka huu.