July 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sheikh Kabeke akerwa na wanasiasa wanaomtukana Rais Samia

Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

SHEIKH wa Mkoa wa Mwanza,Alhaji Hasani Kabeke,amewashangaa viongozi wa dini kukaa kimya wakati baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wasio na maadili wakimtukana na kumdhalilisha Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.

Pia,amewataka Waislamu na wasio Waislamu wenye sifa kujitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufinyika mapema mwaka huu.

Sheikh Kabeke katika hotuba ya Eid Al Adhaa iliyoswaliwa Juni 17 mwaka huu katika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza,ambapo amesema viongozi wa dini wako kimya ili hali Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, akidhalilishwa kwa matusi na baadhi ya vyama vya siasa na viongozi wasio na maadili, hivyo watoke wakemee jambo hilo.

Alhaji Kebeke amesema Rais Samia hatazamwi kama chama bali ni taasisi na nembo ya nchi ni lazima aheshimiwe na heshima yake ilindwe na Watanzania wote, kumtukana ni kumdhalilisha binafsi,familia na taasisi yake ya Urais.

Kwa mujibu wa Sheikh huyo wa Mkoa amesema tabia hiyo ikiendelea BAKWATA haitawaunga mkono viongozi wasio na maadili na vyama vyao,itawashauri waumini wake na wengine kuvikataa vyama hivyo na viongozi wao.

“Rais ni taasisi hatuzungumzii kama chama bali nembo ya nchi,hatuwezi kuunga mkono viongozi wasio na maadili ama sivyo tutawashauri waislamu wawakatae,”amesema.

Sheikh Kabeke amewashauri viongozi wengine wa dini kukemea tabia hiyo ya matusi na udhalilishaji.

Akizungumzia uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu,amesema wenye sifa waislamu na wasio waislamu wakajisajili katika daftari la wapiga kura wakachukue fomu wagombee uongozi.

“Mwaka huu ni wa uchaguzi wa serikali za mitaa wenye sifa na nafasi waende kwenye vyama wakajisajili,siku ya kupiga kura chagua kiongozi anayekufaa,usichague chama ama vyama visivyo na maadili,”ameshauri.

Kwa upande wa mmomonyoko wa madili Sheikh huyo wa Mkoa wa Mwanza,amesema dunia inalalamika kukosa maadili kwa sababu wanaopaswa kuyajenga yawezekana walikutana katika mitadao ya kijamii,facebook,whatsApp na twitter sasa X na unapotaka kuoa oa mwanamke mwenye dini anayemcha Mungu.

“Wapo watu leo hawawaheshimu wazazi wao,tunapomtafuta mtoto tumwombe Mungu atupatie mwenye maadili,maadili hayawezi kutengenezwa ndani ya umri wa miaka 30 na kiwanda cha kutengeneza watoto wema wenye maadili ni ndoa iliyobarikiwa na Mwenyezi Mungu,isiyotokana na kukutana kwenye mitandao ya kijamii,”amesema Sheikh Kabeke.

Aidha amewataka waislamu wasikubali kugawanywa kwa itikadi za dini zao,wajenge umoja na mshikamano ili kufikia maendeleo ya kiuchumi na kijamii,bila umoja na mshikamano ni vigumu kuyafikia.

Pia amesistiza kulinda amani ya nchi akisema; “Ujumbe huu ufike, tuendelee kulinda amani ya nchi na bila amani leo tusingeswali hapa, dini yetu ni ya amani na mwislamu unapotembea unatangaza amani,tusikubali kuivunja amani yetu tuendelee kuilinda.