December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Shaka awataka wanahabari kufichua ufisad, matumizi mabaya ya madaraka

Na Penina Malundo, TimesMajira Online

CHAMA Cha Mapinduzi CCM kimesema kuwa vyombo vya Habari viendelee kufichua na kupiga vita vitendo vya ufisadi, vikemee ubadhirifu wa mali za umma, wizi na kushamirisha mapambano dhidi ya adui rushwa na matumizi mabaya ya madaraka kwa viongozi wa Umma.

Huku kimesisitiza kuwa kitahakikisha kuwa, Uhuru wa Vyombo vya Habari unaimarishwa na kulindwa huku wamiliki na wanahabari wanazingatia maadili na weledi katika kazi zao.

Akizungumza hayo leo katika kuadhimisha siku ya Habari Duniani,Katibu wa Nec Itikadi na Uenezi Taifa wa Chama hicho,Shaka Hamdu Shaka amesema CCM na Serikali zake zinatambua na kuheshimu Vyombo vya Habari na Waandishi wa Habari kwani Tasnia hiyo ina msukumo na mchango mkubwa wa maendeleo ya Taifa.

Shaka amesema Chama cha Mapinduzi (CCM) kinawataka wanahabari kutimiza majukumu ya kufichua badala ya kuficha ukweli kwa kuzingatia maadili na miiko ya kisheria iliyopo.

Amesema hata Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais Tanzania Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza kuwa angependa kusikia habari za kweli zikiwafikia Wananchi kwa haraka mahali popote walipo mijini au vijijini.

Amesema na hiyo ndiyo maana hivi karibuni aliielekeza Serikali kuzifungulia TV za mitandaoni na kuwataka wamiliki na wahariri wao kufuata Sheria, kuheshimu maadili ya uandishi wa habari na kuzingatia Kanuni zake, kama ilivyosisitizwa katika Ilani ya Uchauzi ya CCM kuwa,chama kitahamasisha matumizi ya Mitandao ya Kijamii ili kuongeza upatikanaji wa habari” 6(125h).

Amesema tasnia ya Habari inapokuwa huru na Waandishi wakiandika kwa uwazi, uhalisia na ukweli na kutumia kalamu zao kwa weledi na maadili husaidia kuharakisha maendeleo.

Amesema pamoja na Uhuru wao, Vyombo vya Habari na Waandishi wanatakiwa kuzingatia na kuheshimu Sheria za nchi, kufuata Maadili, Miiko na Kanuni za Taaluma ya Uandishi wa Habari unaojenga nchi badala ya kalamu zao kupotosha au kuchochea mifarakano.

“Chama Cha Mapinduzi kama ilivyoahidi katika Ilani ya Uchaguzi (2020 – 2025) Sura ya 06, Fungu la 125, kitaendelea kuzielekeza Serikali zake kuheshimu Tasnia ya Habari huku tukiwahimiza Waandishi wa Habari kuandika Habari zitakazojenga nchi badala ya zile za kulibomoa Taifa,amesema na kuongeza

“Tunavikumbusha Vyombo vya Habari Kutambua vina haki na wajibu wa kuielimisha jamii ,vitoe elimu kwa Wakulima mashambani na Wafanyakazi viwandani,kalamu zao zisiache kuandika ukweli kuhusu maendeleo ya kilimo, mifugo, madini, uwekezaji, afya na jamii ya Watanzania, lakini vikosoe na kurekebisha kama kuna haja ya kufanya hivyo,”amesema

Aidha amesema Chama kitafanya kila linalowezekana kuimarisha Vyombo vya Habari vya Chama ili vifikishe habari za kisera na kimaendeleo kwa haraka na kwa uhakika katika jamii kwaninVyombo vya Habari na Waandishi wa Habari wana kazi na wajibu wa kuelimisha, kufundisha na kuburudisha jamii.

Shaka amesema Chama kinafurahi pale Waandishi wa Habari wanapoandika kwa kuzingatia weledi katika Tasnia yao baada ya kupata Habari kutoka vyanzo ama mamlaka husika na si habari za kuifarakanisha jamii.